Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limeeleza kusikitishwa na taarifa iliyochapishwa na gazeti la Tanzania Daima iliyohusisha kuadhimishwa miaka 52 ya Jeshi hilo na tukio la kisiasa la Septemba 1 mwaka huu.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, JWTZ limesema kuwa gazeti hilo lilichapisha habari hizo katika toleo lake la Septemba 1 mwaka huu, katika toleo namba 4290.

“Jeshi ni taasisi ya dola wala si taasisi ya kiitikadi, kwa maana uhusiano wake na wanasiasa ni wakati linapotetea na kulinda maslahi ya wananchi.  Inaombwa kuwa makini katika utoaji wa maelezo au malalamiko, iachwe mara moja vyama vya siasa kuingilia ratiba za Kijeshi,” imeeleza taarifa ya JWTZ.

Aidha, imewataka wanasiasa kusoma vizuri historia ya nchi kwani kwa kufanya hivyo wangekuwa wametambua uwepo wa Septemba 1 kama siku ya kuanzishwa kwa Jeshi hilo, tofauti na Julai 25 ambayo ni siku ya kuwakumbuka Mashujaa  wa Taifa.

Jeshi hilo limewataka wanasiasa kuwa makini na lugha wanazotumia huku likionesha kukerwa na baadhi ya matamko ya kisiasa yaliyotolewa yakilihusisha jeshi hilo na masuala ya kisiasa.

“ugha na maneno yanayotolewa na viongozi wa kisiasa wenye matakwa binafsi kuhusisha shughuli za Jeshi na siasa zao yanatia ukakasi na kiungulia, awe makini kuongea vitu ambavyo haelewi na kutokuwa makini zaidi aelewe madhara yanayoweza kutokea kutokana na upotoshaji,” imeeleza taarifa hiyo.

Awali, Septemba 1 ilitajwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kuwa ni siku watakayofanya maandamano na mikutano nchi nzima kupitia Oparesheni waliyoiita UKUTA, lakini tarehe hiyo iliingiliana na ratiba ya JWTZ lililotangaza kufanya usafi mitaani katika kuadhimisha kuanzishwa kwake. Chadema ilitangalitaza kuahirisha nia yao siku moja kabla ya siku hiyo.

Aliyemuua Mpenzi wake kwa visu ashinda taji la ‘Urembo Jela’, ajuta
Picha: Majaliwa atembelea Muhas- Mloganzila