Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limetoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Tabora kufanyakazi kwa ushirikiano na uzalendo ili kuimarisha ulinzi wa eneo lao na nchi kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi Meja Jenerali, Sharif Othman wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa wa Tabora na Wilaya zake wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo.

Amesema kuwa ushirikiano utawasaidia kuwafanya kuwa kitu kimoja na kuwa na nguvu ya pamoja katika kuhakikisha usalama na ulinzi wa wananchi na nchi kwa ujumla.

Meja Jenerali Othman amesema viongozi wa vyombo hivyo wanapaswa kujenga tabia ya kutembelea na kushirikiana katika shughuli mbalimbali kama vile michezo na sherehe kama sehemu ya kujenga mshikamano ambao ndio utawasaidia kuwa kitu kimoja katika ulinzi wa nchi.

Aidha, amesema hali hiyo itawasaidia kupeana taarifa kama kutakuwepo na jambo ambalo linahatarisha usalama wa nchi na hivyo kuchukua hatua za pamoja na haraka katika kulikabili.

“Sisi tuwe mashine ya kuwezesha usalama wa raia na nchi kwa kupeana taarifa na kushirikiana,” amesema Meja Jenerali Othman.

Ameongeza kuwa, sio vyema kungoja tatizo litolekee ndio taarifa itolewe bali taarifa inapaswa kutolewa mapema ili kuzuia tatizo.

Makamu wa Rais mgeni rasmi tamasha la Urithi Festival
Mbunge Jumaa atoa misaada jimboni kwake