Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema katika Baraza Jipya la Mawaziri ameamua kuwaacha kando Prof, Palamagamba Aidan Kabudi na William Lukuvi kwa ajili ya kumsaidia kazi maalumu Ikulu.

Rais Samia ameyasema hayo leo Januari 10, 2022, katika uapisho wa mawaziri na manaibu waziri wateule aliowateua mwisho wa Juma lilipota akifanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri.

Rais samia amesema kuwa wawili hao, kutokana na umri na busara zao ameona wanafaa kuwa washauri kwa viongozi vijana walioteuliwa na kumsaidia kufanya maamuzi ya Ikulu.

“Nimeshasikia jumbe mbalimbali zinawachoma huko hawa kaka zangu kuwa ooh wameachwa, hawafai, Hapana! Hawa wamekaa muda mrefu kwenye Baraza na wanajua kila eneo, hivyo nimeamua kuwapa kazi ya kuja kwangu kuwasimamia nyie vizuri,” alisema.

“Kakaangu Kabudi amefanya kazi nzuri sana ya kusimamia Serikali na Mashirika, na ndio kazi ambayo nataka nimkabidhi sasa kindakindaki aendelee n kazi hiyo. Ila kazi yake kwa sababu haiko kwenye Muundo haitangazwi wala nini lakini atasimamia hiyo kazi. Mashirika yote na kazi zote zitakazoingia ubia na Serikali Kabudi ataongoza hiyo timu. Kwa hiyo yeye ni baba mikataba.” Aliongeza Rais Samia.

Aidha amesema kuwa Lukuvi ana kazi maalumu Ikulu ambayo kwa sasa hakuitaja na akiufahamisha umma kuwa itafahika baadae.

“Wengine wameanza kumletea meseji za ajabu ajabu wakidhani atagombania uspika, hatagombania! Ana kazi na mimi kwa hiyo hatakuwa spika wala hatagombania, msianze kumchafua. Ametumikia nchi hii kwa mda mrefu na kwa uadilifu msianze kumchafua muache aende na mimi tumalize kazi tutakayompangia.” Alisema Rais Samia.

Katika Mawaziri na Manaibu wapya walioapishwa hii leo wapo ambao ni wapya walioingia kwa mara ya kwanza na wapo ambao walibadilishwa kutoka wizara moja kwenda wizara nyingine.

Kilichojitokeza zaidi katika mabadiliko baraza la mawaziri yaliyofanywa na Rais Samia ni kuundwa kwa Wizara Mpya ambayo ni Wizara maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum, wizara hii itaaongoozwa na Waziri Dorothy Gwajima ambaye alikua waziri wa Afya.

Nape Nnauye ndiye Waziri mpya wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, alikotoka Dkt Kijaji. Nape aliwahi kuongoza Wizara ya Habari na kuondolewa mwaka 2017 na Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.

Kwa upande wa manaibu Ridhiwani Kikwete ameteuliwa kuwa naibu waziri wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi. Antony Mavunde Naibu wizara ya kilimo, Jumanne Sagini naibu waziri wizara ya mambo ya ndani. Lemomo Kiruswa ambaye ni naibu waziri wa Madini, na Atupele Mwakibete naibu waziri wizara ya ujenzi na uchukuzi.

Naibu waziri mwingine aliyepandishwa cheo ni Agelina Mabula atakayeongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya Makazi kuchukua nafasi ya William Lukuvi, mwanasiasa mkongwe aliyedumu katika nafasi za juu serikali kwa muda mrefu na pia ni mbunge wa Ismani mkoani Iringa kwa zaidi ya miaka 25.

Mawaziri waliobakia katika nafasi zao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberatha Mulamula; Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba; Waziri wa Nishati, January Mkamba; Waziri wa Madini, Doto Biteko; Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro; Waziri wa Maji, Jumaa Aweso; Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa; Waziri wa Ulinzi, Stegomena Tax; na Waziri Ofisi ya Rais – Kazi Maaalum, George Mkuchika.

Mbowe arejeshwa Mahakamani baada ya mwaka Mpya
Wezi wapika vyakula na kujisaidia ndani ya kanisa