Aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila amedai kuhujumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuwekewa urasimu wa kupata fomu za matokeo ya uchuguzi huo ili aweze kuzitumia kama ushahidi katika kesi yake ya kupinga ushindi wa Hasna Mwilima wa CCM.

Kafulila amewaambia waandishi wa habari kuwa amekuwa akizungushwa na NEC kupata fomu za majumuisho ya matokeo ya uchaguzi huo na kupigwa danadana za maelekezo ya viongozi wa ngazi juu wa Tume hiyo.

Alieleza kuwa Novemba 12 alimuandikia barua msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo kuomba fomu hizo lakini aliambiwa zimetumwa makao makuu ya NEC, hali iliyomlazimu kufuatilia.

“Zilipita siku 10 bila majibu. Novemba 24 nilionana na Kailima na alipewa maelekezo na Jaji Damian Lubuva (Mwenyekiti wa NEC). Kailima alimpigia simu msimamizi msaidizi wa jimbo na kumtaka anipe fomu hizo kupitia msaidizi wangu,” alieleza Kafulila.

Aliongeza kuwa licha ya kutolewa kwa maagizo hayo, hadi kufikia jana alikuwa bado hajapata fomu hizo ambazo ni ushahidi muhimu mahakamani.

Kafulila anaeleza kuwa tarehe alizokuwa anapigwa danadana na NEC zinaonesha kama kuna mpango wa kuandaa fomu mpya wakati uchaguzi ulishapita na fomu zilikuwepo na kilichotakiwa ni kumkabidhi tu.

“Ilinishangaza, iweje waandae fomu wakati fomu hizo sio za kuandaliwa na ziko tayari kwa sababu uchaguzi ulishafanyika?” Kafulila anakaririwa.

Hata hivyo, maelezo ya Kafulila yalipingwa na Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima ambaye alidai kuwa hawawezi kumpatia fomu hizo kwa sababu Msimamizi wa uchaguzi hawezi kumpa ushahidi mlalamikaji bali atauwasilisha mahakamani.

Kailima alisema kuwa mawakala wa Kafulila walipewa fomu namba 21B kutoka katika kila kituo cha kupigia kura na fomu namba 24B kutoka katika kituo cha majumuisho ya kura.

“Fomu hizo zina matokeo ya kila kituo na katika kituo cha kujumlisha kura zote. Mawakala wa Kafulila walipewa, sasa anataka tumpe zipi? Kama amefungua kesi yeye awasilishe malalamiko yake na msimamizi atawasilisha huo ushahidi wake,” alisema Kailima.

Kafulila amefungua kesi mahakamani akiitaka Mahakama kumtangaza kuwa mshindi wa ubunge kwa madai kuwa fomu namba 21B za matokeo ya vituo vyote zinaonesha amepata kura 234,212 dhidi ya kura 33,390 alizopata Mwilima.

Msimamizi wa uchaguzi alimtangaza Mwilima kuwa mshindi wa uchaguzi huo baada ya mvutano ambapo Kafulila alipinga kuhesabiwa upya kwa kura kwa madai kuwa mabox ya kura yalilala katika kituo cha polisi. Kwa mujibu wa matokeo rasmi, Mwilima alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata kura 34,453 dhidi ya kura 33,382 za Kafulila.

 

 

Magumashi: Utashangaa Kilichomkuta Baba Wa Watoto Wawili Alipoenda Kupata Huduma Ya Tiba Mbadala
Rais Magufuli awaapisha Mawaziri na Manaibu Waziri Waliokuwa Wamesalia