Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, David Kafulila amesitisha mkataba wa ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Mkoa na ya Katibu Tawala Mkoa uliokuwa kati yake na Shirika la Ujenzi la Taifa (TBA), kutokana na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo.

Kafulila akiambatana na wakuu wa Sehemu wa Sekretarieti ya Mkoa wa Songwe amefikia uamuzi huo mara baada ya kutembelea eneo la ujenzi wa nyumba hizo na kukuta hatua ya ujenzi iliyofikiwa hairidhishi.

Amesema kuwa kasi ya ujenzi wa nyumba hizo inatia mashaka kutokana na kuwa kazi iliyokwisha fanyika kwa muda wa siku sitini ni ndogo ukilinganisha kazi na muda uliobakia kufikia tarehe ya makubaliano ya kukamilika ujenzi.

“Kazi iliyobaki kiuhalisia haiwezekani TBA wakaikamilisha kwa muda uliobakia, kwani tuliwakabidhi eneo la ujenzi tarehe 2-2-2019 na tulikubaliana ikifika tarehe 30-06-2019 nyumba hizo mbili ziwe zimekamilika lakini kwa kipindi cha miezi miwili hakuna kitu wamefanya na kuna dalili zote za kutokamilisha kwa muda,” amesema Kafulila.

Ameongeza kuwa TBA wamekuwa na tabia ya kutekeleza miradi ya ujenzi kwa kasi ndogo mkoani Songwe na hivyo kusababisha fedha kurudishwa hazina kuu kutokana na kutozitumia kwa muda unaotakiwa yaani ndani ya mwaka wa fedha wa serikali ambapo fedha hizo zinakuwa zimetolewa.

Aidha, amesema kuwa Mkoa hauna matatizo na Wizara ya Ujenzi wala shirika hilo la TBA ila lazima hatua za kusitisha mkataba huo zichuliwe ili kunusuru fedha hizo kurudishwa hazina kuu kutokana na kuchelewa kuzitumia ndani ya mwaka wa fedha wa serikali pia ili nyumba hizo zikamilike kwa muda na kuwezesha makazi ya viongozi.

Hata hivyo, ameongeza kuwa gharama ya Ujenzi wa Nyumba ya Mkuu wa Mkoa ni shilingi milioni 499.9 na tayari TBA walipewa malipo ya awali ya shilingi milioni 74.9 huku nyumba ya Katibu Tawala Mkoa ikiwa na gharama ya shilingi milioni 499.7 na malipo ya awali yaliyotolewa ni shilingi milioni 74.9

 

Juhudi za serikali kupiga marufuku mifuko ya Plastiki ziungwe mkono
Video: HATARI HII...! Shuhudia MAZISHI YA AJABU ZAIDI Duniani