Rais wa Rwanda, Paul Kagame amekubali kumsaidia Rais Mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta kuwahimiza waasi wa M23 kuweka silaha chini na kujiondoa katika maeneo waliyoyanyakua na kuyadhibiti, ambapo mbinu za kufanikisha hatua hiyo zitajadiliwa wakati wa duru ya pili ya mazungumzo katika mji mkuu wa Angola Luanda wiki kesho.

Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, imebainisha kuwa Kenyatta na Kagame wamekubaliana juu ya haja ya waasi wa M23 kusitisha mapigano na kujiondoa katika maeneo ya mashariki mwa Kongo, ambapo Rais wa Angola, Joao Lourenco alikuwa mpatanishi wa mkutano wa kwanza kati ya maafisa wa Kongo na Rwanda mapema mwezi huu (Novemba, 2022).

Uhuru Kenyatta (kushoto), na Paul Kagame. Picha ya Ikulu ya Kenya/ Twitter.

Waasi wa M23 wamekuwa wakiendesha mashambulizi kadhaa mashariki mwa Kongo DRC, wakirejea kwao kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012, na kusababisha makabiliano na jeshi la Kongo na ambapo maelfu ya raia wamelazimika kuyahama makazi yao tangu mwezi Machi.

Machafuko hayo, yalizua mvutano wa kidiplomasia kati ya Kongo na nchi jirani ya Rwanda, ambayo Kongo inaituhumu kuwaunga mkono waasi hao, tuhuma zinazokanushwa vikali na Rwanda. Juhudi za kikanda zinaendelea ili kurahisisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili na kujaribu kuumaliza mzozo unaoendelea karibu na mpaka wa Kongo na Rwanda.

Tangazo la Serikali lasababisha mauaji Gerezani
Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Novemba 19, 2022