Klabu ya Kagera Sugar imetamba kuiangamiza Simba SC katika mchezo wa Kiporo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaounguruma kesho Jumatano (Januari 26), katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.

Mchezo huo ulipaswa kuchezwa Desemba 12 mwaka 2021, lakini uliahirishwa na Bodi ya Ligi kutokana na wachezaji wengi wa Simba SC kukutwa na maambukizo ya ugonjwa wa mafua, kukohoa, kichwa na homa kali, hivyo kusababishwa mechi isifanyike kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Kagera Sugar wametamba kushinda mchezo huo kupitia Ukurasa wao wa Instagram kwa kundika maneno ya kuwataka mashabiki na wanachama wa Simba SC kujiandaa kwa majonzi mengine baada ya kuambulia kisago cha bao 1-0 dhidi ya Mbeya City kisha matokeo ya sare 0-0 dhidi ya Mtibwa Sugar.

“Hapa kuna watu walizimia jukwaani baada ya Juma Kaseja kupangusa mkwaju wa penati ya Emmanuel Okwi, tukutane Jumatano Kaitaba, mtu apigwe tena na kitu kizito kichwani.”

“Magari ya wagonjwa yatakuwapo ya kutosha kutoka hospitali zote za mkoa wa Kagera, kwa hiyo nyie zamieni tu.” Ni maneno yaliyoandikwa kwenye mtandao rasmi wa instagram wa klabu ya Kagera Sugar.

Simba SC tayari imeshaondoka jijini Dar es salaam mapema leo Jumanne (Januari 25) kuelekea mjini Bukoba tayari kwa mchezo huo, huku ikiwa na alama 25 zinazoiweka katika nafasi ya pili kwenye msimamo, na Kagera Sugar ikiwa nafasi ya 11 kwa alama 13.

Simba SC yaifuata Kagera Sugar
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Januari 25, 2022