Mshambuliaji wa mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC, Meddie Kagere amewakumbusha wachezaji wenzake kuwa, hategemei kuona wakipoteza nafasi ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.

Kagere ametoa kauli hiyo baada ya kuwasili nchini jana, akitokea nchini kwao Rwanda tayari kwa kuungana na wenzake kwa ajili ya kumalizia michezo iliyobaki ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (ASFC).

Mshambuliaji huyo anaeongoza kwa kupachika mabao msimu huu, amesema kuwa uwepo wao kileleni mwa msimamo wa Ligi ni fursa muhimu ambayo hawatakiwi kuipoteza.

“Siamini kwamba kuna mchezaji yeyote ambaye ameshafika juu halafu akakubali kuanguka. Kama uko juu uko juu huwezi kukubali kulipoteza,” amesema Kagere.

Hata hivyo Kagere amesema kuwa kutokana na ligi kusimama kwa muda mrefu bila wachezaji kucheza, kuna kazi kubwa inayopaswa kufanyika ili wawe na ubora waliokuwa nao kabla ligi na mashindano mengine hayajasimamishwa na serikali kama miongoni mwa hatua za kukabiliana na virusi vya Corona.

“Kilichotokea kwa wachezaji kimetuathiri kwa sababu tumekaa kwa muda mrefu bila kucheza mechi. Kama unataka kuwa uko levo ya juu, jambo la kwanza ni kuwa na ufiti wa mechi.”

“Ufiti wa mechi ni ishu ya kila mchezaji huwezi kufanya mazoezi kwa miezi miwili lakini ukiukosa kwa kutocheza mechi au za kirafiki sikatai kwamba inaweza kuwa na athari kwa kila mchezaji na inahitajika mechi mbili au tatu urudi katika kiwango chako cha kawaida.”

“Programu na yale yote tuliyoelekezwa wakati wa mapumziko nimeyafanya kama nilivyohitajika na nimeyatekeleza inavyotakiwa.Nilikuwa nazungumza nao (makocha) wakajua maendeleo yangu,” alisema Kagere.

Katika hatua nyingine, Kagere amesema uamuzi wa michezo iliyobakia kuchezwa bila uwepo wa mashabiki viwanjani, utapunguza hamasa kwa wachezaji.

“Haiwezi kuwa kama tulivyozoea. Kikubwa kutakuwa na mabadiliko kwa sababu hakutokuwa na watu wakija mazoezini, uwanjani kutokuwa na watu wachache kinyume na vile tulivyozoea kwamba watu wanajaa uwanjani na kutushangilia,” alisema Kagere.

Simba inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na alama 71 na inahitaji ushindi katika michezo mitano tu kati ya 10 iliyobakiza ili itetee ubingwa ambao utaifanya iwe imechukua taji hilo kwa misimu mitatu mfululizo.

Amuuza mwanae baada ya kufukuzwa nyumbani
Zlatan ajiweka pembeni AC Milan