Kocha Mkuu wa Singida Big Stars, Hans Van de Pluijm amesema kutokuwepo kwa nyota wa kikosi chake cha kwanza, Meddie Kagere na Said Ndemla ambao wameitwa kwenye vikosi vya timu zao za taifa hakuwezi kumpa hofu na presha kwani ana wachezaji kibao wanaoweza kutimiza majukumu yao vyema na kuwapa ushindi kesho dhidi ya Geita Gold.

Singida Big Stars itaivaa Geita Gold kesho Septemba 21 saa 10 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza baada ya mchezo huo uliopaswa kupigwa Septemba 14 kusogezwa mbele kuipa muda Geita Gold kujiandaa na mchezo wao wa kimataifa.

Akizungumzia mchezo huo kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini hapa leo, Pluijm amesema nyota hao wawili ni muhimu ndani ya kikosi chake lakini hapaswi kunung’unika kwani timu yake ina chaguo pana la wachezaji wanaoweza kumpa matokeo mazuri.

Amesema Ligi Kuu Tanzania Bara ni mashindano yenye ushindani mkubwa na kila mchezo ni mgumu na Geita Gold ni timu yenye ushindani mkubwa kwani ameifuatilia na kuona ikicheza vyema lakini sasa anawaachia wachezaji kutimiza majukumu yao na kuondoka na pointi tatu.

Amesema mchezo wa kesho ni sawa na michezo mingine ya ligi ambayo timu yake imekwishacheza msimu huu lakini ana imani kubwa ya kushinda kutokana na maandalizi ya mwisho waliyoyafanya leo kwenye mazoezi yao ya mwisho.

“Ninachoweza kusema tunacheza na mpinzani mzuri nimeshawaona wakicheza, bila shaka tunatakiwa kushinda mechi. Kitu kizuri ninachoweza kusema tuko kwenye hali ya ushindi na ndicho ambacho tuko kwa hilo.” amesema Pluijm

Msuva: Tupo tayari kuikabili Geita Gold FC
Wanawake waongoza tatizo la afya ya akili