Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe ameelezea jinsi alivyohojiwa leo na Idara ya Uhamiaji ambapo Idara hiyo imeichukua pasi yake ya kusafiria kwa uchunguzi.

Kakobe amesema kuwa katika mahojiano hayo yaliyojikita katika suala la uraia wake, aliulizwa maswali mengi ili kuthibitisha kama yeye ni raia halali wa Tanzania au la.

Amesema pamoja na mambo mengine, aliulizwa kuhusu vyeti vya kuzaliwa vya wazazi wake.

Kiongozi huyo wa dini ameeleza kuwa kwakuwa anaikumbuka vizuri historia ya utoaji vyeti nchini, alieleza kuwa zoezi la utoaji vyeti la majaribio lilianza miaka ya 1980 tena kwa wilaya 6 pekee. Hali hiyo inaonesha ugumu wa upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa vya wazazi wake ambao ni marehemu.

Aidha, Askofu Kakobe ameeleza kuwa aliulizwa walipozikwa wazazi wake na aliwajibu kuwa makaburi yao yako sebuleni nyumbani kwao.

“Haya mambo kwa sababu yamewahi kutokea miaka ya nyuma, kwa makusudi kabisa wakati baba yangu na mama yangu walipofariki, baba alifariki mwaka 2009 na mwaka 2013… Nilitoa maelekezo kwa ndugu zangu, kwa sababu najua mambo haya na mimi ni mtu wa kusema kweli wakati wote.

“Nikasema tuweke makaburi haya sebuleni. Yaani makaburi ya baba na mama yangu yako sebuleni,” amesema Askofu Kakobe.

Amesema yeye alizaliwa katika kijiji cha Mbizi wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma. Alisoma mkoani humo na baadaye kujiunga na mafunzo ya jeshi kwa mujibu wa sheria baada ya kumaliza elimu ya sekondari.

“Muovu anakimbia hata kama hajafuatwa na mtu lakini mwenye haki huwa jasiri kama Simba,” alisema.

Akizungumzia hatua ya kuchukuliwa kwa pasi yake ya kusafiria, amesema ameambiwa ni kwasababu ya matumizi ya kiofisi na kwamba atarejeshewa ndani ya muda mfupi.

Kakobe alifika katika ofisi za Idara ya Uhamiaji saa nne kamili asubuhi kuitikia wito wa Idara hiyo uliotolewa Ijumaa iliyopita.

Kocha Zamalek ajiuzulu.
Kakobe afunguka baada ya kuhojiwa na uhamiaji