Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam imemuita Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe kwa ajili ya kumhoji.

Hatua hiyo imethibitishwa na Naibu Kamishna wa Uhamiaji Mkoani humo, Crispin Ngonyani alipofanya mahojiano hivi karibuni na mwandishi wa Mwananchi.

Ngonyani alisema kuwa Idara hiyo imemtaka Askofu Kakobe kufika ofisini kwao kesho kwa sababu ambazo hakuziweka wazi kwa madai kuwa ni kazi za ndani za kiofisi. Alisema kazi za Idara hiyo ni pamoja na kuita watu na kukamata watu.

Naye Askofu Kakobe, alisema kuwa amepokea wito huo na atafika katika ofisi hizo ziolizoko ndani ya jengo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kwamba amejiandaa.

“Tayari nimejipanga. Wamesema niripoti saa nne asubuhi kwa hiyo tunatarajia kufika kule kwa wakati ambao wao wameutaka,” alisema Askofu Kakobe na kuongeza kuwa ameelezwa sababu za wito huo ni kuhojiwa.

Kiongozi huyo wa kidini alifanyiwa ukaguzi na Mamlaka ya Mapato Tanzania hivi karibuni na baadaye ripoti yake kutolewa hadharani.

Aidha, Kakobe alipinga baadhi ya taarifa za ripoti hiyo akieleza kuwa zimetolewa kwa mtazamo usio wa haki na kweli kwa lengo la kutaka kumchonganisha na waumini wake.

Hatua ya kuchunguzwa na TRA ilikuja kufuatia kauli yake aliyoitoa kanisani kwake kuwa ‘ana pesa nyingi kuliko Serikali’. Hata hivyo, baada ya kukaguliwa, alibainika kuwa hana akaunti katika benki yoyote.

 

Rais mstaafu ajisalimisha polisi kuanza kifungo cha miaka 12 jela
Video: Marufuku polisi kufyeka mashamba ya Bangi- JPM, Uraia wa Kakobe 'Utata'