Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe amewageukia baadhi ya viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwataka kutubu au chama chao kitazidi kutumbukia shimoni.

Akizungumza leo katika Ibada ya Jumapili kanisani kwake jijini Dar es Salaam, Kakobe ambaye katika siku za hivi karibuni ameonekana katika mikutano kadhaa ya Rais John Magufuli na kupewa nafasi ya kuzungumza, amesema viongozi hao wanaopaswa kutubu ni wale waliowatukana viongozi wa dini.

Kakobe amedai kuwa yeye hajawahi kuwa mwanachama wa Chadema na kwamba aliwahi kuhudhuria tukio moja tu la Chadema mwaka 2015, Mlimani City. Katika tukio hilo, Chadema walikuwa wanachangisha fedha kwa ajili ya kusaidia gharama za uchaguzi mkuu.

Alisisitiza kuwa anawashangaa wanaodai kuwa anaiacha Chadema, kwani hakuwahi kuwa nao hivyo hakuna sehemu ambayo aliwaacha.

“Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, sijawahi kuwa na mazungumzo naye iwe kanisani au nyumbani au mahali popote. Hata katika mkutano ule [wa Mlimani City] nilipokelewa na viongozi wengine kabisa,” Kakobe anakaririwa na Mwananchi.

Askofu Zachary Kakobe akitoa neno katika tukio la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuisaidia Chadema kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu 2015

Alisema hata Saed Kubenea ambaye ni mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chadema, eneo ambalo kanisa lake lipo, hajawahi kuzungumza naye.

Aidha, alisema kuwa amewahi kuhudhuria mikutano na matukio mengi zaidi ya CCM, kuanzia wakati ambapo Yusufu Makamba alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwani alikuwa rafiki yake mkubwa.

Katika hatua nyingine, Askofu Kakobe amedai kuwa yeye hajanunuliwa kama wengi wanavyodai kwani hajawahi kuwa na bei na hana bei.

Amesisitiza kuwa yeye amewahi kusema kuwa ana fedha kuliko Serikali na kwamba hata Mamlaka ya Mapato Tanzania imewahi kueleza wazi kuwa kanisa lake lina fedha nyingi kwenye akaunti, hivyo hanunuliki.

Kauli hiyo imewahi kumuingiza Kakobe kwenye mgogoro mkubwa na Mamlaka, ambapo alijikuta mikononi mwa TRA pamoja na Idara ya Uhamiaji ambapo alihojiwa na kuchunguzwa.

Hivi karibuni, Kakobe aliwaambia waandishi wa habari kwa ufupi kuwa suala la hati yake ya kusafiria kushikiliwa na Idara ya Uhamiaji sio ‘issue tena’.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 28, 2019
Baada ya kumpiga Lopez, Thurman amtaka Manny Pacquiao

Comments

comments