Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ‘TPLB’, imewafutia adhabu Mtunza Vifaa na Mlinda Lango wa Klabu ya Coastal Union, baada ya kufanya marejeo (Review), ya shauri hilo ambalo lilitolewa maamuzi Januri 26.

Mtunza vifaa Mathayo Francis na Mlinda Lango Justine Ndikumana, waliadhibiwa kwa kufungiwa michezo mitatu sambamba na kutozwa faini, kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya kishirikina kabla ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar, uliopigwa Uwanja wa Kaitaba Januari 21-2023.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Bodi ya Ligi ‘TPLB’ imeeleza kuwa, Klabu ya Coastal union iliomba marejeo ya shauri hilo, kwa mujibu wa Kanuni ya 27:4 ya Ligi Kuu kuhusu Vyombo vya Maamuzi.

Katika kikao cha marejeo kamati ilipitia upya shauri hilo na kufanya tena tathmini ya maelezo kutoka vyanzo zaidi, na kujiridhisha kuwa taarifa za awali zilizowasilishwa kwenye kikao chake cha Januari 26-2023 hazikuwa sahihi, hivyo kusababisha kamati kufanya maamuzi ambayo hayakuwa sahihi, pia kulingana na uhalisia wa kilichotokea.

Kutokana na hilo kamati imefanya maamuzi yafuatayo: Mtunza Vifaa wa Coastal Union Mathayo Francis amefutiwa adhabu ya kufungiwa michezo mitatu na kutozwa Fainli ya Shilingi Milioni Moja (1,000,000) kwa madai ya kufanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina.

Pia Golikipa wa timu hiyo Justine Ndukumana amefutiwa adhabu ya kufungiwa michezo mitatu na kutozwa Faini ya Shilingi Laki Tano (500,000).

Kauli ya Chifu yazusha mapigano, 13 wauawa
Ofisi za ardhi zaagizwa kutoa huduma siku zote za juma