Kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji (PIC) imeihoji Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa matumizi ya zaidi ya shilingi bilioni 38 ambayo ni karibu nusu ya mapato yake ya ndani, kwa ajili ya kulipana kwenye semina, safari na shughuli za kiutawala.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Losensia Kukwimba ambaye ni mbunge wa jimbo la Busanda alisema kuwa baada ya kuipitia ripoti ya ya TCRA  ya mwaka 2013/14 wamebaini kuwa shilingi bilioni 18 zilitumika kwa ajili ya semina, safari, mafunzo na kujitangaza (publicity0 na pia shilingi bilioni 20 zikitumika kugharamia kazi za kiutawala. Kiasi hicho kinakaribia nusu ya pato la mwaka la Mamlaka hiyo ambalo ni shilingi bilioni 79.

“Tukiwa kama Kamati ya Uwekezaji na Mitaji, tunaona hiki ni kiasi kikubwa cha matumizi na tunaitaka TCRA kupunguza matumizi hayo na kuelekeza fedha hizo kwenye miradi kwa maslahi ya watanzania walio wengi,” alisema.

Naye mwenyekiti wa Bodi ya TCRA, Profesa Haji Semboja aliiambia kamati hiyo kuwa Mamlaka hiyo ililazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuwajengea uwezo watumishi wake kutokana na kazi zake.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk. Ally Simba alisema kuwa hawakuweza kujikita katika miradi kwakuwa Mamlaka hiyo haikuanzishwa kwa lengo la kufanya biashara.

Antonio Conte Kuanza Na Beki Wa Kitaliano
Dk Shein kufungua leo baraza la wawakilishi akiwa na kitendawili