Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imeridhishwa na utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ya uratibu na uzalishaji wa Takwimu rasmi nchini.

Katika ziara ya Kamati hiyo kwenye ofisi za Makao Makuu ya NBS jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Hawa Ghasia, wajumbe wa kamati hiyo wameipongeza NBS chini ya Mkurugenzi Mkuu wake Dkt. Albina Chuwa kwa kuonyesha weledi na umahiri katika kutekeleza jukumu lake la kuratibu, kuzalisha na kusambaza takwimu rasmi nchini.

Wajumbe wa Kamati walipata fursa ya kujifunza masuala mbali mbali ya kitakwimu pamoja na namna NBS inavyotekeleza majukumu yake ya kila siku.

“Leo wajumbe wa kamati ninayoiongoza kwa pamoja tumejifunza namna mnavyoratibu na kuzalisha takwimu rasmi nchini; tumeridhishwa na kazi nzuri mnazozifanya kwa weledi mkubwa,” amesema Hawa Ghasia.

Hata hivyo, Ghasia ametoa wito kwa NBS kuwapatia wabunge takwimu mbalimbali wanazozalisha na wanazoziratibu ili ziweze kuwasaidia katika kutekeleza wajibu wao kikamilifu wakiwa bungeni na hata nje ya bunge.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NBS Dkt. Albina Chuwa ameishukuru Kamati hiyo kwa kuitembelea ofisi ya Takwimu na kujionea kazi mbalimbali zinazofanyika za uratibu na uzalishaji wa Takwimu rasmi nchini.

 

Odinga kuwania tena urais 2022
Ashley Cole ampa muda Unai Emery