Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72 imeipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu kutokana na Rufaa waliyoikatia Kagera Sugar kwa kumtumia beki Mohammed Fakhi akiwa ana kadi tatu za njano katika mechi baina ya timu hizo Aprili 2, mwaka huu.

Katika mchezo huo ambao Kagera Sugar walishinda mabao 2-1 Uwanja wa Kaitaba, wanadaiwa kukiuka kanuni kwa kumchezesha Fakhi, beki wa zamani wa Simba akiwa anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Ahmed Yahya aliwaambia Waandishi wa Habari jana usiku Uwanja wa Karume, Dar es Salaam kwamba Kamati ilibaini ni kweli Kagera Sugar walifanya kosa hilo la kikanuni na adhabu yake ni kupokonywa ushindi.

Kwa ushindi huo, Simba sasa inafikisha pointi 61 baada ya kucheza mechi 26, wakiendelea kuongoza Ligi Kuu mbele ya mabingwa watetezi, Yanga wenye pointi 56 za mechi 25.

Ikumbukwe Simba iliwasilisha malalamiko ikitaka ipewe ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na Kagera Sugar kumchezesha Fakhi akiwa na kadi tatu za njano katika mechi yao namba 194 iliyofanyika Aprili 2, 2017 Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Katika kikao chake awali Ijumaa iliyopita, Kamati baada ya kupitia malalamiko hayo, iliahirisha shauri hilo hadi leo kujipa muda wa kufuatilia baadhi ya vielelezo kuhusu malalamiko hayo.

Mbwana Samatta Ashindwa Kufurukuta Hispania
Huduma mbovu yaziumbua Kampuni za simu nchini