Kambi ya Rais mteule wa Gambia, Adama Barrow imekanusha vikali taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao jana na kuandikwa na baadhi ya vyombo vikubwa vya habari kuwa amepigwa risasi.

Taarifa hizo zilizothibitishwa kuwa ni ‘uzushi’ zimebainika kuanzishwa na tovuti batili ya ‘Skytrendnews’ uliodai kuwa mtu mmoja alipenya katika safu ya walinzi binafsi wa rais huyo mteule na kumuua kwa risasi. Ilidai kuwa muuaji huyo pia aliwaua walinzi wawili wa Barrow.

Kambi ya upinzani inayomuunga mkono Barrow imeeleza kuwa rais huyo mteule yuko salama katika hotel moja kubwa jijini Banjul pamoja na familia yake na viongozi wengine, akisubiri kuapishwa rasmi Januari 19 mwaka huu.

“Barrow na wajumbe wote wa kambi ya upinzani wako hapa na wanaendelea na mambo yao kama kawaida,” mmoja wa viongozi wa kambi hiyo amekaririwa na mtandao wa JaollowfNews.

“Hizo habari ni uzushi. Zimelenga tu katika kufanya kitu kimoja, kuleta mkanganyiko na taharuki. Gambia inapaswa kupuuza taarifa hizi,” aliongeza.

Barrow ameendelea kusubiri terehe rasmi ya Januari 19 ili aweze kuapishwa kuwa rais mpya wa taifa hilo wakati ambapo rais aliyepo madarakani, Yahya Jammeh amekataa kuondoka madarakani licha ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya taifa hilo kumtangaza Barrow kuwa mshindi wa uchaguzi wa Desemba 1 mwaka jana.

Jumuiya ya Afrika Magharibi ya ECOWAS ikiongozwa na rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari imeendelea kumsihi Jammeh kuondoka madarakani, lakini hakuna matumaini ya rais huyo kushawishika kukubali ukweli na kuzingatia demokrasia.

Hata hivyo, hali imeendelea kuzua taharuki baada ya Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo kutangaza kuwa ataendelea kuwa mtiifu kwa rais Jammeh, huku Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi aliyetangaza matokeo ya urais akikimbilia uhamishoni.

Tanesco hali bado tete
Dhamana ya Lema yatua Mahakama ya Rufaa