Washambuliaji kutoka nchini Zambia Lazarius Kambole na Moses Phiri wametabiriwa kufanya makubwa wakiwa na klabu zao mpya Simba na Young Africans katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu msimu wa 2022/23.

Kambole ambaye alishindwa kutamba akiwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, amesajiliwa na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, huku Moses Phiri aliyetamba na Zanaco FC akisajiliwa na Simba SC.

Kocha Msaidizi wa ZESCO united Noel Mwandilwa amewatabiria wawili hao kufanya maajabu katika Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara iliyoanza rasmi jana Jumatatu (Agosti 15) kwa kusema ni suala la muda.

Mwandilwa ambaye aliwahi kufanya kazi Young Africans akiwa msaidizi wa George Lwandamina na baadae kuwa Kaimu Kocha Mkuu amesema, Washambuliaji hao wana uwezo mkubwa wa kupambana na hana shaka nao juu ya uwezo wao kisoka.

Kocha huyo ambaye juzi Jumapili (Agosti 14) alikua sehemu ya Benchi la Ufundi la ZESCO United wakati wa mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Azam FC, amesema Kambole hapaswi kuchukuliwa kama Mshambuliaji wa kawaida kwa kigezo cha kushindwa kuwika akiwa katika Ligi ya Afrika Kusini ‘PSL’, bali anatakiwa kuheshimiwa na kuaminiwa kama Mshambuliaji hatari.

Kwa upande wa Phiri aliyetua Msimbazi miezi miwili iliyopita amesema, Mshambuliaji huyo ni hatari, kwani hata msimu uliopita alionyesha uwezo mkubwa akiwa na klabu yake ya Zanaco FC.

“Si kwa sababu hakufanya vizuri katika Ligi ya Afrika Kusini ‘PSL’ akiwa na Kaizer Chiefs na hata Tanzania akiwa na Young Africans atafanya hivyo pia, huu ni mpira haiko hivyo. Kambole atafanya vizuri kwa sababu ninamfahamu.”

“Phiri hata msimu uliopita akiwa kwenye Ligi Kuu ya Zambia alifanya vizuri, ninaamini akiwa hapa na kikosi cha Simba SC atafanya vizuri pia, ni suala la muda tu, nina uhakika watanzania wanaopenda soka watakubaliana na mimi.” amesema Mwandilwa

Young Africans inatarajiwa kuanza kutetea taji la Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23 leo Jumanne (Agosti 16) kwa kucheza dhidi ya Polisi Tanzania, huku Mshambuliaji Kambole akiwa sehemu ya kikosi kinachotarajiwa kupambania Ubingwa huo.

Moses Phiri huenda akaanza kuonyesha uwezo wake kesho Jumatano (Agosti 17), pale kikosi cha Simba SC kitakachopambana na Geita Gold FC, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Uingereza yaidhinisha chanjo ya Uviko-19 ya lahaja mbili
Marekani yamtaka Mteule Ruto kufanya kazi na washindani wake