Kampuni tisa za nchini Korea Kusini  zimeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania na kuwekeza katika sekta ya kilimo, viwanda, maji, miundombinu, elimu, afya na michezo.

Wawekezaji hao kutoka kampuni ya Sima textile, ESM, Jusung Solar Engineering, Seongnam City FC, Yeong Yang City Korea,Ulsan Vocational Training, Egis Smart City, MBN wameeleza hayo Septemba 27, 2016 wakati walipokutana na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli.

imgs6609Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi wa makampuni mbalimbali kutoka Korea ya Kusini ambao wamekuja Tanzania kuona fursa mbalimbali za uwekezaji. Kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula

Waziri Mkuu alisema kwamba Tanzania ni sehemu salama kwa uwekezaji ikiwa na fursa za uwekezaji kwenye sekta nyingi kama miundombinu, kilimo na viwanda. Pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji pia aliwahahakishia ulinzi kwenye uwekezaji wao.

Majaliwa amesema Korea ya Kusini inashirikiana vizuri na Tanzania hivyo wanatarajia mengi kutoka nchini huko kupitia wawekezaji hao, ambapo ameeleza pia kuwa wawekezaji hao tayari wamefanya mazungumzo na viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza na kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya miradi minne ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya maji, kiwanda cha nguo, zana kubwa za kilimo na mafunzo ya ufundi.

Mkuu wa Msafara kutoka Makampuni hayo, Son Young Soo amesema amefurahishwa na ziara waliyofanya nchini na wapo tayari kuwekeza  nchini. Na Jihyun Kim wa  kampuni ya Yeong Yang City Korea ambayo inashughulikia masuala ya kilimo cha mbogamboga alisema watawekeza kwenye kilimo hususan cha zao la pilipili na watajenga kiwanda kwa ajili ya usindikaji, huku Mkurugenzi wa Klabu ya Soka ya Seongnam, Suk Hoon Lee amesema klabu yake ipo tayari kuwekeza katika shule ya michezo kwa vijana ili kuongeza kasi ya maendeleo ya soka.

imgs6633

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika  picha ya pamoja na  viongozi wa makampuni mbalimbali ya Korea Kusini ambao wapo nchini kuona fursa  mbalimbali za uwekezaji  nchini. Picha hiyo ilitanguliwa na mazungumzo yaliyofanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Septemba 27. Watatu kulia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  Angelina Mbula.

Big Sam: Najutia Sana Kauli Zangu
Uamuzi wa kesi ya mauaji ya dada wa bilionea kusomwa okt 10