Mwaka 2022 umeanza kwa tabasamu la aina yake kwa Kampuni ya Marekani ya ‘Apple’, ikiwa imeweka rekodi nzito ya kuwa kampuni ya kwanza nchini humo kufikisha thamani ya soko ya Dola za Kimarekani Trilioni 3 ($3 trillion).

Apple iliandika rekodi hiyo mapema jana asubuhi, ikiendeleza ubabe sokoni kwa namna ya kipekee baada ya hisa yake moja kuuzwa kwa $ 182.88 trilioni.

Mafanikio hayo ni makubwa ukilinganisha na mafanikio ya awali ya miaka minne iliyopita, ambapo mwaka 2018 iliongoza kwa thamani ya sokoni ikiwa na $1 trilioni, Agosti 2020 ikaongoza ikiwa na thamani ya soko $2 trilioni, na sasa wamefikia thamani ya $3 trilioni.

Hatua ya mafanikio hayo imetokana na jitihada zilizoongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Apple, Tim Cook za kuhakikisha kampuni hiyo haitegemei zaidi mauzo ya iPhones, iPads na vifaa vingine katika ukuaji wake.

Hivi sasa, Apple imejikita katika biashara ya bidhaa na huduma nyingine ikiwa ni pamoja na ‘aplikesheni’, muziki, eneo la utunzaji wa maudhui mtandaoni (cloud storage) ambayo yameongeza pato lake.  

“Kufikisha thamani ya soko ya $ 3 trilioni ni hatua kubwa na ya kihistoria kwa Kampuni ya Apple, na wanaendelea kuwahakikishia wale waliokuwa wanawasiwasi kuwa ndoto zao ni halisi,” alisema Dan Ives, mchambuzi wa masuala ya hisa nchini Marekani.

Bidhaa na huduma za kampuni ya Apple vimeendelea kupata mafanikio makubwa katika soko la dunia na kila wanapotoa toleo jipya la simu mauzo yake hushika hatamu dhidi ya mauzo ya bidhaa za makampuni mengine shindani.  

Pablo: Nimeshakabidhi ripoti
Kocha Pablo atangaza njaa Mapinduzi Cup