Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba ametoza faini Kampuni ya TANMAT kwa kuikuka Sheria ya Mazingira inayokataza upandaji wa miti ndani mita sitini kutoka katika chanzo cha maji, ambapo ameeleza kuwa kampuni hiyo imevunja sheria hivyo hamna budi kuchukuliwa hatua stahiki ili iwe mfano na kwa wengine.

Waziri Makamba amesema hayo mapema leo Oktoba 21, 2016 mkoani Njombe ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kutembelea mikoa mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kujionea hali ya mazingira na kutoa maelekezo stahiki.

Kampuni hiyo imeagizwa kulipa faini hiyo ndani siku saba na endapo watakiuka hatua kali zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Waziri Makamba pia ameiagiza Kampuni hiyo kuondoa miti hiyo ambayo si rafiki kwa mazingira mapema iwezekanavyo na kuagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwapa ‘Restoration Order’ kurudisha mazingira katika hali yake ya kawaida.

Kwa upande wake Meneja wa Kampuni hiyo inayojishughulisha na upandaji wa miti, Joseph Shirima amekiri kupokea barua zizoelekeza kusitisha uharibifu huo wa Mazingira katika chanzo cha Mto Mbukwa ambacho kinasambaza maji kwa wakazi wengi wa Wilaya za mkoa wa Njombe.

Aidha, Waziri Makamba ameupongeza uongozi wa mkoa wa Njombe kupitia Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Rehema Nchimbi kwa kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanachi kuacha kulima bustani za mbogamboga pembezoni mwa mito.

Dkt. Nchimbi alimfahamisha kuwa kwa sasa kuna kikundi kijulikanacho kwa jina la ‘Jerusalemu’ kinachotoa mafunzo kwa wananchi juu ya matumizi bora ya ardhi na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira ambapo lengo ni kuanzisha vituo kama hivyo vya mafunzo kwa Halmashauri zote za Mkoa huo.

Waziri Makamba alitembelea na kuona ‘vinyungu’ ambavyo awali vilikua vikilimwa kando ya mito na kwasasa vimehamishiwa majumbani, katika kuunga mkono jitihada hizo njema Waziri Makamba amechangia mifuko Hamsini ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa darasa litakalotumika kutoa mafunzo zaidi ya kilimo.

2

Bustani darasa ya mbogamboga maarufu kwa jina la ‘vinyungu’ inayozingatia uhifadhi wa mazingira kwa kutolimwa pembezoni mwa chanzo cha maji.

 

3

Wakazi wa Kijiji cha Owadi Maheve ambao wanajishughulisha na kilimo cha mbogamboga kwa kufuata utaratibu wa kutolima kwenye vyanzo vya maji. Waziri Makamba amechangia mifuko hamsini ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa darasa litakalotumika kufundishia njia bora zaidi za kilimo.

Waziri Makamba anaendelea na ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya mazingira nchini, na tayari amewasili katika Mkoa wa Mbeya.

Makamba atangaza ‘Mbeya Mountain Range’ kuwa eneo nyeti la mazingira
Manji: Kama Akilimali Hajalipa Ada Haruhusiwi Kushiriki Mkutano