Ripoti ya nusu mwaka ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), inayobainisha hali ya haki za binadamu nchini, imezinduliwa leo Agosti 20, ambapo imeonyesha kuwepo kwa ushamiri wa hali ya ukatili dhidi ya watoto wadogo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, ambapo amesema kuwa ripoti hiyo ilijikita katika makundi matatu ikiwemo Haki za kiraia na kisiasa, Haki za kijamii pamoja na Haki za makundi maalumu wakiwemo Watoto, Wanawake na watu wenye ulemavu.

”Kwanza kumeendelea kushamiri kwa hali ya ukatili kwa watoto, hasahasa ukatili wa kingono, ubakaji, ulawiti na ukatili wa kimwili dhidi ya watoto, kanda inayoongoza ni Kanda ya Ziwa kwa asilimia 38, ikifuatiwa na kanda ya nyanda za juu Kusini asilimia 32, Pwani asilimia 9, Kaskazini asilimia 9, kanda ya kati asilimia 7 na Kanda ya Magharibi  asilimia 5,” amesema Mkurugenzi Mtendaji LHRC.

Aidha, ripoti hiyo pia imeeleza kuwa, licha ya kupungua kwa kiasi kidogo kwa mauaji yanayotokana na imani za kishirikina na kujichukulia sheria mikononi lakini bado hofu imetanda kwa watu wenye Ualbino hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.

”Kumekuwa na kuongezeka kwa hofu miongoni mwa watu wenye Ualbino hasa wakati huu Tanzania inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, sababu kihistoria mwaka wa kuelekea uchaguzi mkuu wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili,” amesisitiza Anna Henga LHRC

UVCCM Dar yataka 2020 wabunge wasipewe fomu mpaka wapimwe
Marekani yafanya jaribio la silaha za Nyuklia