Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ametoa siku 15 kwa kampuni saba zilizobainika kufanya ufisadi katika mradi wa mfumo wa utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kurejesha Sh28.5bilioni walizolipwa, ili kuepuka kuwa wateja wa mahakama ya mafisadi.

Ameyasema hayo jijini Dodoma ikiwa ni siku moja  baada ya kukutana na wamiliki wa kampuni hizo kuomba wawasilishe vielelezo vya malipo hayo.

Lugola amezitaja kampuni hizo kuwa ni Gotham International Ltd (Sh2.8 bilioni), Iris Corporation Berhard (Sh22.9 bilioni), Gwiholoto impex Ltd (Sh 946.4 milioni), Skyes Travel Agent (Sh6 milioni), Dk Shija Paulo Rimoy (Sh27 milioni), Aste Insurance (Sh1.2 bilioni) na BMTL (Sh 569.1 milioni) ambayo imekubali kurejesha fedha hizo.

“Takwimu nilizonazo mahakama ile ya mafisadi bado ina uhaba wa mafisadi, mimi nina dhamana ya kuitafutia wateja. Nyinyi tuliohojiana muombe msiwe miongoni mwa wateja ninaoitafutia mahakama hiyo, na msilete mchezo na serikali hii ya awamu ya tano”, amesema Lugola

Aidha, kuhusu hatima ya aliyekuwa mkurugenzi wa Nida, Dickson Maimu na kampuni ya Iris Corporation Berhard ya nchini Malasia ambayo ililipwa Shilingi bilioni 32 na Nida kwa ajili ya kuleta mtambo wa kutengenezea kadi ghafi nchini, amesema itajulikana Agosti 17, 2018.

Hata hivyo, Ufisadi huo katika mradi wa mfumo wa utambuzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), uligundulika katika ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya  Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Februari, 2016

Moise Katumbi amkalia kooni Rais Kabila
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Agosti 5, 2018