Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amemuagiza Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Arusha kumuondoa Mkuu wa Kituo cha Polisi Mang’ola wilayani Karatu kwa kushindwa kusimamia misingi ya kazi.

Amefikia uamuzi huo wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Karatu katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini humo, ambapo amesema kuwa malalamiko yaliyotolewa na wananchi wilayani humo yanaonyesha kuwa Mkuu huyo wa Kituo ameshindwa kusimamia nidhamu.

“RPC nakuagiza umuondoe haraka iwezekanavyo Mkuu huyu wa Kituo hiki, mlete mwingine atakayejenga nidhamu upya ya askari katika kuwahudumia wananchi wa Mang’ola kwani kumekuwa na malalamiko mengi yanayotolewa na wananchi juu ya askari kushindwa kusimamia misingi ya kazi yao,” amesema Lugola.

Aidha, katika hatua nyingine, Lugola amemwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Karatu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, wafike katika Gereza la Mang’ola wilayani humo, kuwaonyesha uongozi wa gereza hilo, eneo la kuchimba mtaro wa maji ili waachane na mtaro wanaoutumia wananchi ambao umekuwa ukileta mgogoro ndani ya eneo hilo.

Pia Waziri Lugola amemuagiza Mkuu wa Magereza Mkoa wa Arusha kuwaondoa askari watatu waliolalamikiwa kuwazuia wananchi kutumia maji na kuwapiga wananchi.

Wakizungumza katika mkutano huo wa hadhara, baadhi ya wananchi walitoa malalamiko jinsi askari magereza walivyowanyanyasa kwa kuwatisha kwa kutumia bunduki huku wakiwataja kwa majina yao kuwapiga raia na kuwanyang’anya upataji wa maji wakati wao sio wahusika wa zamu katika siku vitendo ambavyo vimefanya kuibua mgogoro mkubwa.

Serikali yalaani vikali mauaji ya watoto
Majaliwa amtumbua Mweka Hazina Kibondo