Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ameipa wiki mbili Kampuni ya Kimataifa ya Iris Corporation Berhard impe majibu ya kuwa italeta mtambo wa kutengeneza kadi ghafi au Dola za Marekani Milioni 14 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 32 za Tanzania.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma mara baada ya kumaliza kikao na Menejimenti ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) pamoja na viongozi wa Kampuni hiyo.

Lugola amesema kuwa kampuni hiyo haiwezi ikacheza na fedha za Watanzania ambao ni za walipa kodi.

Amesema kuwa lazima fedha hizo au mtambo huo upatikane kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitakubaliana na mchezo mchafu wa aina yoyote, na pia yeye kama Waziri wa Wizara hiyo anaendelea kutekeleza maagizo ya Rais Dkt John Magufuli.

“Tumezungumza nao na tumekubaliana nao kwamba tuwape wiki mbili ili bodi ya kampuni hiyo ikakae ifanye maamuzi ya aidha waturudishie fedha zetu au walete mtambo, lakini sisi kama nchi, huu mtambo ni muhimu sana, bado tuna uhitaji, sisi tungependa baada ya hiyo wiki mbili wafanye maamuzi ya kutuletea mtambo,” amesema Lugola.

Aidha, Lugola amewataka wamiliki wa kampuni zilizolipwa kifisadi fedha za Mradi wa mtambo wa NIDA kujisalimisha jijini Dodoma Agosti 3 mwaka huu wakiwa na mtambo huo vinginevyo warejeshe fedha zilizotumika.

Hata hivyo, Lugola ameyataja makampuni hayo kuwa ni Gotham International ambayo imelipwa kifisadi shilingi 2,848,878,659.75, Iris Corporation Berhard ambayo imelipwa kifisadi 22,919,414,169,84, Gwiholoto Impex inayodaiwa shilingi 946,406,989,00, Sykes Travel Agent 5,979,600,00, Dk. Shija Paul Rimoy 27,000,000,00, Aste Insurance 1,206,619.93, na Kampuni ya BMTL 569,192,090,00.

 

Video: Chadema waamsha kifo cha Akwilina, Waziri Lugola aibua ufisadi mpya NIDA
Babu Tale afunguka ya Mavoko na WCB, ‘akishiba anasogea pengine’