Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amepokea fedha taslimu shilingi milioni 10 kutoka Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) zikiwa ni msaada kwa ajili ya watu waliopatwa na maafa kutokana na tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Majaliwa amepokea mchango huo nyumbani kwake, Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Majaliwa amesema anawashukuru sana viongozi wa dini zote kwa jinsi wanavyoisadia Serikali kuwahudumia wananchi kupitia sekta mbalimbali.

“Tunatambua juhudi zinazofanywa na taasisi za dini zote kuunga mkono juhudi za Serikali, tunafarijika mno na tunawashukuru sana,” – Majaliwa.

Amemuomba Askofu huyo pamoja na viongozi wengine wa dini wawaombee kwa Mungu viongozi waliopo madarakani ili awape hekima na busara na awawezeshe kuwaongoza vema Watanzania.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT, Dk. Brown Mwakipesile wakati akikabidhi mchango huo amesema kanisa hilo limeona lina wajibu wa kuisadia Serikali kuwapunguzia machungu watu waliopatwa na maafa kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu 17.

“Tumeona ni vema kanisa la EAGT lishiriki kuisadia Serikali kuwafariji wananchi waliopata maafa kutokana na tetemeko hilo. Tumeona ni wajibu wetu kwa sababu waliopatwa na maafa ni watu wetu wote. Tunawaombea wote waliopatwa na shida waweze kupata nafuu mapema zaidi,” amesema.

Mbali na hilo, Askofu Mwakipesile amesema ameona jinsi Serikali ilivyosimamia vizuri suala la madawati hadi sasa kuna baadhi ya maeneo wamevuka hadi malengo. Hivyo amemshukuru Rais Magufuli na Serikali nzima kwa kusimamia jambo hilo vizuri.

Amesema kanisa hilo linatoa shukrani nyingi kwa Rais Dk. John Pombe Magufuli kwa jitihada zinazofanywa na Serikali yake kukabili mambo mbalimbali yanayowagusa wananchi walio wengi.

Tetemeko hilo la ardhi liliharibu miundombinu ya barabara, shule, zahanati na kujeruhi watu 440. Pia lilisababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi na 9,471 zikipata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada.

 

Nchemba atumia Jamii Forums kutoa ufafanuzi kuhusu kupotea Msaidizi wa Mbowe
Video: Mbowe maji ya shingo, Mrithi wa Lubuva NEC afunguka...