Watu 13 wamefariki dunia na wengine wamejeruhiwa baada ya Kanisa la Kipentekoste (Pentecostal) kuanguka jana usiku, April 18 katika eneo la Angubo, KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa Serikali ya KwaZulu-Natal, kanisa hilo lilianguka kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikiendelea kunyesha kaskazini mwa jimbo hilo.

Msemaji wa kitengo cha matibabu ya dharura, Robert McKenzie amesema kuwa watu sita wamepata majeraha makubwa na wengine 10 wamepata majeraha madogo.

Msemaji wa polisi wa jimbo hilo, Colonel Thembeka Mbele amesema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa mvua kubwa yenye upepo mkali iliyonyesha katika eneo hilo ndio chanzo kikuu cha tukio hilo.

Hadi leo asubuhi Polisi walikuwa katika eneo la tukio ambapo watu takribani 29 walipelekwa hospitalini, kwa mujibu wa News24.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, watu walikuwa wamelala ndani ya kanisa hilo wakati ukuta wa kanisa ulipoanguka usiku wa manani.

Mahakama yabariki kuondolewa ukomo wa umri wa kuwania Urais
Lissu: Nitarejea, sitakubali kuishi uhamishoni