Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na kumhakikishia kwamba Ujerumani iko tayari kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania hususani kusaidia kuimarisha uchumi.

Angela Merkel amempongeza rais Magufuli kwa juhudi anazozifanya na serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga mazingira mazuri ya uwekezaji ikiwemo kupambana na rushwa na kuimarisha miundombinu.

Amesema kuwa Ujerumani itawaleta wafanyabiashara watakaowekeza katika maeneo mbalimbali ya kuimarisha uchumi ikiwa ni pamoja na kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea ambacho kitakuwa kikubwa kuliko vyote barani Afrika.

Aidha, amesema kuwa Ujerumani imedhamiria kuunga mkono juhudi za ujenzi wa viwanda nchini Tanzania na kwamba ana matumaini makubwa kwamba kiwanda kitakacho jengwa kitaweza kuinua uchumi.

Kwa upande wake, Rais Magufuli amemshukuru Kansela Angela Merkel kwa kumpigia simu na kuonyesha dhamira yake ya kukuza zaidi uhusiano wa Tanzania na Ujerumani na kuhakikisha kuwa Tanzania inajenga mazingira mazuri ya ushirikiano yakiwemo ya biashara na uwekezaji.

Hata hivyo, rais Magufuli amempongeza Angela Merkel kwa uongozi wake wa zaidi ya miaka 13 wa kuiongoza Ujerumani, huku akimhakikishia kuwa Tanzania itadumisha na kukuza ushirikiano kati ya nchi hizo.

CCM yaja na mpango mkakati ya kukiimarisha chama
Mr Beneficial: Yale ni maisha nimewahi kuyaishi Arusha