Mlinda lango na Nahodha wa KMC FC Juma Kaseja amesema kwa sasa hakuna timu bora nchini Tanzania kama Simba SC.

Kaseja ameukubali mziki wa Simba SC, huku akikumbukia kichapo cha mabao 2-0, kilichowafika Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi Jumatano (Julai 07).

Mlinda lango huyo ambaye amewahi kuzituminia Simba SC na Young Africans kwa nyakati tofauti amesema kama kuna mdau anapinga kuhusu ubora wa kikosi cha Mabingwa hao wa Tanzania Bara atakuwa mnafiki wa mchana kweupe.

Amesema Simba SC imekamilika kila idara na unapocheza nayo unaona ubora wake, hivyo hana budi kutoa sifa hizo hadharani.

“Tukubali au tukatae Simba ni bora kwa sasa, timu nzuri na wachezaji wazuri ambao tayari walishapevuka na mkifanya makosa wachezaji hao lazima watawaadhibu,” amesema Kaseja.

Simba SC inahitaji alama moja pekee kujihakikishia utetezi wa taji lake msimu huu, baada ya kuifunga KMC FC mabao 2-0, juzi Jumatano (Julai 07).

Simba SC itacheza dhidi ya Coastal Union keshokutwa Jumapili (Julai 11), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Mchezo wa mzunguuko wa kwanza uliozikutanisha timu hizo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Simba SC iliibugiza Coastal Union mabao 7-0.

Bilioni 20 za Mo zazua tena mjadala mitandaoni
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Julai 9, 2021