Aliyekua Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa wa Mtwara, Aziz Mrope amevuliwa nafasi hiyo pamoja na kufutiwa uanachama wa umoja huo baada ya kubainika kuwa amedanganya umri.

Uamuzi wa kumvua madaraka  umetolewa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James baada ya mkutano wa umoja huo kupitisha maamuzi hayo  jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari James, baada ya kumaliza mkutano huo amesema kuwa uamuzi umefikiwa na  mkutano mkuu kujiridhisha kuwa Mrope alifanya udanganyifu kwenye umri.

” Kwa umoja wetu ambayo tumejadili katika Mkutano mkuu tumeridhia kwa pamoja kumfuta uanachama Bw.Mrope kwa udanganyifu na tumemuondoa katika nafasi yake ya uongozi aliyokuwa nayo, hivyo niuagize Mkoa wa Mtwara kuanza mara moja mchakato wa kujaza nafasi hiyo ambayo ipo wazi,” Amesema Kheri.

Katika hatua nyingine James amewapongeza viongozi wa Mikoa wa UVCCM na wanachama wao kwa kuhakikisha kuwa CCM inashinda kwa kishindo kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24 mwaka huu.

Amewataka kuendelea kutangaza kazi kubwa inayofanywa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe Rais Dk John Magufuli ili kumtengenezea njia rahisi ya kupata kura nyingi katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020.

Jonathan Pitroipa: Naikabidhi The Stallions kwa vijana
Aliyembaka bibi wa miaka 60 atupwa jela miaka 30