Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) imesema kuwa mchakato wa kupigia kura za maoni katiba mpya inayopendekezwa umeanza baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva amesema kuwa Tume hiyo ilisimamisha mchakato wa kura za maoni kwa Katiba Mpya inayopendekezwa ili iweze kushughulikia Uchaguzi Mkuu na sasa imeurejesha mezani kwa ajili ya utekelezaji.

“Tulikuwa tunangoja tumalize uchaguzi. Kama vile ambavyo Mnyamwezi anavobeba mzigo, unamaliza mmoja unakwenda kwa mwingine. Sasa tumemaliza uchaguzi mkuu tunakwenda kwa lingine,” alisema Jaji Lubuva.

Alieleza kuwa mchakato huo unahitaji bajeti kubwa, hivyo wananchi watajulishwa muda ukifika kuhusu hatua zinazoendelea.

Taarifa hii ya NEC inakuja wakati ambapo vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa vimekuwa vikisisitiza kuwa Katiba hiyo irudishwe kwenye hatua za majadiliano ili kuibeba Rasimu ya Tume ya Warioba, huku upande wa Chama Cha Mapinduzi wakionesha kuiunga mkono kwa asilimia zote.

Wakati akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza, Rais Magufuli alieleza kuwa anatambua kuwa ana kiporo cha Katiba Mpya na kwamba atalisimamia ipasavyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo atimuliwa, mamilioni yapotea hovyo
Msanii wa Afrika ashinda Tuzo ya Grammy kwa mara ya tatu