Rais John Magufuli amewatumbua Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Amantius Msole  na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Steven Makonda. baada ya viongozi hao, kubainika kufungua akaunti nyingine inayofanana na ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Maafa ya Kagera iitwayo “Kamati Maafa Kagera”   kwa ajili ya kujipatia fedha

JPM ameagiza vyombo vya dola, vichukue hatua kwa kila aliyehusika. Sambamba na hilo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Simbaufoo Swai kutokana na kuhusika katika njama hizo.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, kwa vyombo vya habari jana ilieleza hayo.

Hata hivyo, Majaliwa ametoa mwito kwa wananchi na taasisi mbalimbali, kuendelea kuchangia misaada kwa ajili ya walioathirika kwa kutumia akaunti rasmi ya “Kamati Maafa Kagera” ambayo imetangazwa na Serikali.

Wakati huo huo, Dk Magufuli amepokea msaada wa Sh milioni 545 kutoka kwa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi kwa ajili ya kusaidia wananchi wa mkoa wa Kagera waliopatwa na maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka huu.

Hundi ya fedha hizo imekabidhiwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam na Balozi wa India nchini, Sandeep Arya na baadaye Rais Magufuli akaikabidhi kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Katika barua yake kwa Rais Magufuli iliyosomwa na Balozi Arya, Modi alisema Serikali na wananchi wa India, wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa maafa hayo, yaliyosababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali.

“Tunaziombea amani na uvumilivu familia zote zilizopatwa na madhara na pia tunapenda kuwahakikishia kuwa tupo pamoja na marafiki zetu Serikali ya Tanzania katika kipindi hiki kigumu” alisema.

“Naomba unifikishie shukrani zangu za dhati kwa Waziri Mkuu Modi, mwambie kwa niaba ya Serikali yangu tunamshukuru sana kwa kutoa msaada huu muhimu kwa ajili ya watanzania wenzetu waliopatwa na maafa kule Kagera…,” “…Mwambie ameonesha moyo wa upendo na ushirikiano kwetu na tumefarijika kwamba marafiki zetu mmeguswa kwa namna ya kipekee na tatizo lililoipata nchi yetu” alisisitiza Rais Magufuli.

 

 

 

Mzimu Wa Kevin de Bruyne Wamtesa Pep Guardiola
Big Sam: Najutia Sana Kauli Zangu