Siku moja baada ya kuondoka Mtibwa Sugar na kujiunga na Ihefu FC kama mkuu wa benchi la ufundi, kocha mzawa Zubeir Katwila ametoa neno la shukurani kwa waajiri wake wa zamani.

Katwila amehudumu Mtibwa Sugar kama mchezaji tangu mwaka 1999, na baadae kuwa kocha mkuu wa timu ya kampuni hiyo inayosazilisha Sukari mkoani Morogoro.

Kocha huyo amesema hana budi kuwashukuru viongozi wa Mtibwa Sugar kwa mazuri waliomtendea wakati wote akiwa klabuni hapo, na anaimani matunzo na mafunzo waliyompatia ndio chagizo kwake la kuonwa na viongozi wa Ihefu FC.

 “Nashukuru uongozi wa Mtibwa kwa kuniamini kwa kipindi kirefu nimekuja hapa kama mchezaji 1999 naondoka hapa nikiwa nimepewa majukumu ya  ukocha hakika wamekuwa walezi bora kwangu, Mtibwa ipo ndani yangu na mtibwa ni nyumbani” amesema kocha huyo.

Anaondoka Mtibwa Sugar huku akiacha kumbukumbu ya kutwaa ubingwa wa kombe la Mapindizi msimu uliopita kwa kuifunga Simba SC bao moja kwa sifuri, sambamba na kufanikiwa kuipigania klabu hiyo isishuke daraja.

Aliipeleka Mtibwa Sugar kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika msimu wa 2018/19, baada ya kutwaa ubingwa wa kombe la Shirikisho Tanzania Bara kwa kuifunga Singida United mwishoni mwa msimu wa 2017/18.

Katwila ataanza kazi yake kesho kwenye mchezo wa Ligi Kuu, ambapo kikosi cha Ihefu FC kitakua na shughuli pevu ya kuikabili Azam FC kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Sokione jijini Mbeya.

Jela miaka 20 kwa kukutwa na nyamapori
Mzawa aweka rekodi Ligi Kuu 2020/21