Kufuatia kifo cha bondia maarufu nchini, Thomas Mashali kugubikwa na taarifa nyingi ambazo zimezua mijadala isiyo na majibu ya uhakika, rafiki wa karibu wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Ally amesimulia mkasa mzima baada ya kumsikia marehemu akieleza kabla ya kifo chake.

Ally alisimulia mkasa wa rafiki yake huyo jana alipokua msibani maeneo ya Tandale jijini Dar es salaam, ambapo amedai kuwa juzi usiku alipata taarifa za kushambuliwa kwa Mashali na watu wasifahamika maeneo ya Kimara jijini humo.

Amesema taarifa hizo alifikishiwa na madereva wa Pikipiki (Bodaboda) akiwa nyumbani kwao eneo la Mabibo, ndipo alipoamua kwenda eneo la tukio na kumkuta rafiki yake akiwa na hali mbaya lakini tayari askari polisi walikua wameshafika.

“Nilifika eneo la tukio lakini kwa bahati mbaya nilikuta askari wanampakia Mashali katika Defender (aina ya gari) na mimi nilifuatilia gari hilo kwa nyuma hadi katika hospitali ya Sinza Palestina,” Ally alisimulia.

“Alipatiwa kitanda na nilibahatika kuzungumza nae japo alikua hatoi sauti vizuri, nilimsikiliza kwa tabu baada ya kumuuliza chanzo cha yaliyomfika.  Aliniambia alikodisha pikipiki (Bodaboda) na walikubaliana na dereva angemlipa elfu tatu (shilingi 3,000)  lakini walipofika njiani yeye (Mashali) alitaka ashushwe, baada ya kushushwa alilipa elfu mbili (shilingi 2,000) tofauti na makubaliano yao ya awali,” alisimulia.

Ally anasema Mashali alimwambia kuwa kile kitendo cha kutoa pesa ndogo kinyume na makubaliano kilimkasirisha yule Bodaboda na wakaanza kubishana, ndipo Mashali aliyekuwa amelewa akaanza kumpiga makonde yaliyompeleka chini.

Alisema kuwa Mashali alimwambia kuwa kelele zile za Bodaboda zilisababisha watu watatu kufika eneo la tukio na kuanza kuhoji, lakini Mashali aliyekua amepandwa na hasira na akaanzisha ugonvi na wote watatu akaanza kuwashambulia na kuwazidi nguvu pia.

“Wale jamaa walivyona hivyo waliungana na yule dereva wa bodaboda kupiga kelele za mwizi na ndipo raia wengine walipokusanyika na kumshambulia na vitu vizito, nakumbuka aliniambia alihisi amepigwa na kitu kizito mfano wa rungu eneo la nyuma ya kichwa akahisi kuishiwa nguvu na kuanguka chini,” rafiki huyo wa Mashali anakaririwa.

Ally alizungumzia tukio hilo kwa uchungu huku akisema Mashali alikua rafiki yake wa karibu sana, na kuondoka kwake duniani amemuachia ukiwa.

Katika hatua nyingine, baba mzazi wa Mashali amesema wameamua kufanya mazishi siku ya Jumatano ili kuwapa nafasi Polisi kufanya uchunguzi.

“Tumewaachia kidogo polisi wamalizie kazi yao, lakini mazishi yatakuwa Jumatano badala ya Jumanne kama ilivyokuwa hapo,” alisema.

Msiba wa bondia huyo ambaye ameuwawa na watu wasiojulikana upo kwao Tandale jijini Dar es Salaam.

Muigizaji wa 'Empire' ajiunga Timu Davido
Bilionea wa Unga 'El Chapo' asimulia mateso anayopata gerezani