Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa mbunge wa jimbo la  Nkasi Kaskazini, Aida Khenani, aliyeshinda katika uchaguzi mkuu alikula kiapo cha nafasi hiyo kinyume na msimamo wa chama chake.

Amezungumza hayo kupitia channel ya Youtube ya chama hicho na kusema kuwa, mbunge huyo pamoja na madiwani wengine zaidi ya 80 walioshinda na kula kiapo, kosa walilolifanya si la jinai bali walienda kinyume na taratibu za chama na msimamo wa chama hicho ambacho kinaamini kuwa uchaguzi haukufanyika.

“Watanzania wenzangu mbunge wetu wa Nkasi Kaskazini na baadhi ya madiwani wameapa na kuingia kwenye vyombo vya kiserikali kinyume na msimamo wa chama, nguzo kuu ya chama chochote cha kisiasa ni nidhamu, bila hivyo chama hugeuzwa kuwa genge la wahuni lisilo na miiko wala mipaka”, amesema Mbowe

“Baada ya uchaguzi mkuu tofauti na wabunge wa viti maalum, mbunge wetu wa Nkasi na madiwani kadhaa hawajatenda jinai bali walikaidi ama walikataa kuheshimu msimamo wa chama na chama kitafanyia kazi mazingira ya kila mmoja wao, kitawasikiliza na kuchukua uamuzi stahiki kwa wakati mwafaka zaidi“, amesema Mbowe.

Itakumbukwa katika Uchaguzi mkuu uliofanyika Octobar 28, 2020 CHADEMA ilipoteza karibu majimbo yote nchini na kushindi kwa mbunge wa jimbo moja la Nkasi Kaskazini.

Bilionea Jack Ma adaiwa kutojulikana alipo
Mbunge wa Marekani aapa kuingia na bunduki Bungeni