Kwa mara ya kwanza aliyekua kocha mkuu wa Young Africans ameushauri Uongozi wa klabu hiyo, baada ya kuonyeshwa mlango wa kutokea usiku wa kuamkia jana Jumatatu.

Kaze aliondolewa Young Africans na wasaidizi wake, baada ya mambo kumuendea kombo kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania kwa kulazimishwa sare ya 1-1 dakika za lala salama, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Kaze amewashauri viongozi wa Young Africans kwa kuwaambia kuwa, endapo wanahitaji kuwa kikosi bora ni lazima wahakikishe wanafanya usajili wa kuboresha zaidi kikosi hicho kwa kuwa kwa sasa hakijitoshelezi.

Akizungumzia kufutwa kwake kazi, Kaze amesema: “Tangu nilivyofika Yanga nilisema wazi kuwa miongoni mwa matatizo makubwa tuliyokuwa nayo ni kutokujitosheleza kwa kikosi tulichokuwa nacho.”

“Ni kweli viongozi walijitahidi kufanya usajili mzuri mwanzoni mwa msimu, lakini bado hatukuwa na wachezaji wenye daraja bora ambao wanaweza kuziba pengo la mchezaji yeyote anayecheza ndani ya kikosi cha kwanza ‘deep bench’ iwapo anakosekana.

“Hii ndiyo maana majeruhi yalikuwa adui mkubwa kwetu, kwani nyota waliokuja kuchukua nafasi za majeruhi hawakuweza kutupa kile kitu tunachokihitaji.

“Lakini hata dirisha dogo viongozi walijitahidi kusajili lakini kwa bahati mbaya huwezi kubadilisha wachezaji nane kwenye dirisha dogo, lakini ili kuwa bora ni lazima Yanga isajili wachezaji wa kuweza kupambana na nyota wanaoanza kwenye kikosi cha kwanza,”

Mpaka anaonyeshwa mlango wa kutokea juzi usiku, Kaze alikuwa ameiongoza Young Africans kwenye jumla ya michezo 25, akishinda michezo 16, amefungwa michezo miwili na kutoa sare mechi saba.

Kati ya michezo hiyo 25, michezo 18 ni ya Ligi Kuu Bara, michezo minne ni ya kombe la Mapinduzi, michezo miwili ya kirafiki na mchezo mmoja ni wa kombe la Shirikisho la Azam maarufu, kombe la FA.

Francis Baraza anukia Kagera Sugar
Wasanii waipongeza konyagi kwa kutambua jitihada za wanawake