Wakati kiungo kutoka Angola, Carlos Fernandes ‘Carlinhos’ akitua nchini leo Agosti 25, Kocha Mkuu mpya wa Young Africans, Mrundi Cedric Kaze anatarajiwa kuwasili Ijumaa.

Kiungo Carlinhos anayejiunga na Young Africans akitokea G.D. Interclube ya Angola, yeye ametua leo wakati mshambuliaji raia wa Burkina Faso, Sogne Yacouba akitokea Klabu ya Asante Kotoko ya Ghana, akitarajiwa kutua keshokutwa, Al-Khamisi.

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, ambao ni wadhamini wa Klabu ya Yanga, Mhandisi Hersi Said, amewataka Mashabiki na wanachama wa Young Africans kutarajia mambo mazuri msimu ujao wa Ligi Kuu ambao utaanza rasmi mwishoni mwa juma lijalo.

“Tumebakiza usajili wa wachezaji wawili ambao mmoja ametua leo,  Wanayanga waendelee kuuamini uongozi wao na watarajie mazuri kwa msimu mpya wa 2020/21.”

Kuhusu kocha mkuu, Hersi amesema ataanza safari Alhamisi akitokea Canada na kuwasili nchini Ijumaa, tayari kuanza kuinoa timu hiyo ambayo msimu huu imefanya usajili mkubwa zaidi pengine katika historia ya klabu hiyo.

“Tayari amekamilisha taratibu zote na Al-Khamisi ataanza safari ya kuja nchini kuanza kuinoa timu yetu,” amesema Hersi ambaye amesimamia usajili wote wa Yanga msimu huu.

Kuhusu Yacouba, amesema kuwa kinachomchelewesha mshambuliaji huyo kutua nchini ni kutokana na anga la kwao bado kuwa limefungwa kufuatia mlipuko wa virusi vya corona, lakini sasa wanamatarajio ya kumpokea Alhamisi.

“Yeye anatarajiwa kutua Alhamisi kwani viwanja vya ndege vya kwao vilitarajiwa kufunguliwa Agosti 25 (leo Jumanne), hivyo hadi Al-Khamisi atakuwa amewasili,” amesema.

Wachezaji wengine wa kigeni wapya waliosajiliwa Young Africans msimu huu ni pamoja, mshambuliaji Mghana Michael Sarpong ambaye sasa atawania namba na Yacouba pamoja na washambuliaji wazawa, Ditram Nchimbi na Waziri Junior.

Katika nafasi ya kiungo wapya waliosajiliwa mbali na Carlinhos  ni viungo wawili kutoka Klabu ya AS Vita ya DR Congo, Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda, hivyo kuifanya Yanga hadi sasa kusajili jumla ya nyota wapya watano.

Katika hatua nyingine, kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi Jumapili wiki hii, kitakachofanyika Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Young Africans wamepania kuwakuna mashabiki wao vilivyo kwa burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiongozwa na msanii nguli wa Bongo Fleva, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’.

Messi aliteka soko la Italia
Safari ya JPM kugombea Urais