Kesi ya shambulio la kudhuru mwili inayomkabili kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto, imeanza kusikilizwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi Mkoa wa Shinyanga na kuomba msaada wa wakili.

Kazimoto ameshitakiwa kwa kosa la kumshambulia mwandishi wa habari  wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Mwanahiba Richard na kesi yake ilianza kusikilizwa jana.

Akisomewa shitaka hilo,  Mwanasheria  wa Serikali, Upendo  Shemkole, alisema mshtakiwa  alitenda  kosa hilo Februari  10, mwaka huu  katika Uwanja wa CCM Kambarage, mjini Shinyanga,   muda mfupi baada ya kumaliza mazoezi na timu yake ya Simba.

Hata hivyo, mshitakiwa  huyo alikana  shitaka hilo na kuiomba  mahakama  kumpatia mwezi  mmoja ili atafute wakili  wa  utetezi  wake,  ombi  ambalo  lilikubaliwa.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama  hiyo, Rahim  Mushi,  anayesikiliza  kesi  hiyo,  alisema  kesi  imeahirishwa  hadi  Machi  21  mwaka huu,  itakaposikilizwa tena, ili kutoa fursa  kwa mshitakiwa  kupeleka  wakili wake.

Jumla ya mashahidi sita wanatarajiwa  kutoa  ushahidi  mahakamani hapo katika  kesi hiyo,  ambapo  pia alipewa  dhamana ya Sh  500,000.

African Lyon Wajipanga Kufanya Usajili Wa Haja
Arsenal, FC Barcelona Kurejesha Bunduki Zao Uwanjani