Na Sheila Ally, Shinyanga

Kiungo wa Simba, Mwinyi Kazimoto amefikishwa katika kituo kikuu cha Polisi cha Shinyanga kwa kosa la kumshambulia mwandishi wa gazeti la michezo la Mwanaspoti linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communication, Mwanahiba Richard baada ya mazoezi yao yaliyofanyika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga leo.

Tukio hilo lilitokea mara baada ya Simba kumaliza kufanya mazoezi kwenye uwanja huo huku chanzo cha mgogoro huo kikisemwa kuwa ni madai ya Kazimoto kuandikwa vibaya na mwandishi huyo baada ya mechi zao mbili zilizochezwa jijini Mbeya kati ya Simba  na Mbeya City na Prisons.

Habari inayodaiwa kuandikwa ni juu ya Mwinyi na wachezaji wengine kutuhumiwa kucheza chini ya kiwango kwenye mechi hiyo na kwamba watachunguzwa ili kujua chanzo cha wao kucheza chini ya kiwango.

Baada ya tukio hilo, mwandishi huyo alikwenda kutoa taarifa katika kituo cha Polisi cha wilaya na kupewa hati ya kukamatwa kwa Kazimoto (RB) yenye namba SHY/RB/895/2016 pamoja na fomu ya matibabu (PF3) kisha akapelekwa hospitali ya Mkoa kwa ajili ya matibabu.

Simba inakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Stand United siku ya Jumamosi huku Kazimoto akiwa amejihakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha kocha Jackson Mayanja, tukio hili linaweza kumwathiri katika maandalizi ya mchezo huo muhimu.

Alipoulizwa mwandishi huyo alikiri kushambuliwa na Kazimoto na kusema kwamba suala hilo sasa lipo chini ya vyombo vya sheria hivyo anasubiri sheria ifuate mkondo wake.

Shujaa: Mwanamke Tarime awanyang’anya Majambazi Watatu Bunduki yenye Risasi
Wasira akosoa muundo wa wizara za Magufuli, adai hana uhakika kama unabana matumizi