KCB Bank Tanzania imengia mkataba na Shirikisho la soka nchini TFF wa kudhamini Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (VPL) kwa msimu wa mwaka 2018/2019. Mkataba huo wenye thamani ya shilingi za Kitanzania 420,000,000 umetiwa saini leo Jumatatu na Mkurugenzi Mtendaji wa KCB Bank, Cosmas Kimario na Rais wa TFF  Wallace Karia katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

KCB Bank Tanzania imeongeza thamani ya udhamini wake kwenye ligi hiyo kutoka kiasi cha shilingi za Kitanzania 325,000,000 msimu wa 2017/18 mpaka shilingi 420,000,000 msimu wa 2018/19 ongezeko la ziadi ya milioni 90,000,000, ongezeko linaloashiria dhamira ya benki hiyo kutaka kunyanyua vipaji na kuendeleza ushindani katika mpira wa miguu nchini Tanzania.

Hafla ya kutia saini makubaliano hayo ilihudhuriwa pia na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya KCB Bank Tanzania, Fatma Chillo, Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura, Wakurugenzi wa Bodi na wafanyakazi KCB Bank Tanzania, wawakilishi wa vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya soka na waandishi wa habari.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kusainiwa mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa KCB Bank Tanzania, Cosmas Kimario alisema kwamba mchango wa kiuchumi unaoletwa na soka ni mmoja sababu kubwa zilizopelekea KCB Bank Tanzania kutaka kudhamini ligi hiyo kwa Mwaka wa pili mfululizo. “Tunaamini kuwa sekta ya michezo ina mchango mkubwa katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini kwani ni chanzo cha ajira kwa watanzania hasa vijana.” alisema Kimario.

Kaimu Menyekiti wa Bodi ya KCB Bank Tanzania, Fatma Chillo alisema kuwa ni fursa ya kipekee kuweza kudhamini Ligi Kuu Tanzania bara kwa msimu wa pili. “Lengo letu ni kuleta hamasa kwa timu na mashabiki wa mpira wa miguu kwa kuzijengea timu, hata zile ndogo uwezo wa kifedha ili kuziwezesha kushindana kikamilifu hivyo kuongeza ushindani ndani ya ligi.” Alieleza Bi. Chillo.

Naye Rais wa TFF, Wallace Karia aliishukuru KCB Bank Tanzania kwa kuidhamini Ligi kuu Vodacom jambo ambalo alisema litasaidia kufanikisha msimu huu wa ligi kuu 2018/19. Pia alizitaka taasisi zingine na watu binafsi kuiga mfano huo kuweza kutoa michango ya hali na mali ili kukuza maendeleo ya soka kwa timu za ligi kuu.

Kabla ya kusaini mkataba mpya, KCB Bank Tanzania walikua wadhamini wenza katika ligi kuu ya soka Tanzania bara msimu wa 2017/18, huku mdhamini mkuu akiwa kampuni ya mawasilino ya Vodacom Tanzania ambayo mkataba wake na TFF ulifikia kikomo mwishoni mwa msimu uliopita.

 

Robert Lewandowski awekewa vikwazo FC Bayern Munich
Video: Mapenzi, ugomvi katika familia, nyumba za kupanga ni sumu ya ndoto ya mtoto wa kike katika elimu