Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umetajwa kuwa nguzo muhimu katika uimarishaji wa huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Hospitali ya Kanda KCMC, Gileard Masenga alipokuwa akizungumza na Maofisa Uhusiano wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, ambapo amesema kuwa mchango wa NHIF umekuwa ni mkubwa katika upande wa mapato pamoja na uimarishaji wa miundombinu na vifaa tiba.

“Kwa kweli niseme ukweli kabisa NHIF kwetu ni uti wa mgongo katika uendeshaji wa shughuli zetu na ndio maana kila siku nikikutana na Mkurugenzi Mkuu Konga huwa namwambia watulindie sana huu Mfuko maana umekuwa mkombozi mkubwa sana katika sekta ya afya,” amesema Dkt.  Masenga.

Amesema kuwa maboresho makubwa yaliyofanywa katika eneo la wagonjwa wa dharula hospitalini hapo yanatokana na NHIF,ambapo kwasasa wagonjwa wanapata huduma katika eneo zuri na lenye nafasi ikilinganishwa na awali.

Kwa upande wa Meneja wa wa NHIF Mkoa wa Arusha, Isaya Shekifu amesema kuwa Mfuko umekuwa na mpango wa uimarishaji wa miundombinu na upatikanaji wa vifaa tiba kupitia fursa ya mkopo nafuu kwa lengo la kuboresha huduma za matibabu.

Hata hivyo, naye Afisa Uhusiano wa NHIF,  Grace Michael ametoa wito kwa wananchi kujiunga na huduma za Mfuko ili wawe na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote.

Video: Ugaidi tena Kenya, Magufuli akerwa atoa tamko zito
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Januari 16, 2019