Bondia machachari ambaye hajawahi kupoteza pambano kati ya mapambano yake 29, Keith ‘One Time’ Thurman ameahidi kumuondoa kwenye ulimwengu wa masumbwi, bondia mkongwe, Manny Pacquiao.

Pacquiao na Thurman wanatarajia kuzichapa ulingoni, Juni 20 mwaka huu nchini Marekani.

Jana, katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu pambano hilo uliofanyika nchini Marekani, Thurman aliahidi kumpa kipigo cha mbwa koko Pacquiao na kwamba atahakikisha anamstaafisha.

“Nitampiga, nitamzimisha na naahidi baada ya pambano hili hatapigana tena ulingoni,” Thurman alitamba. “Mayweather aliyekuwa Mfalme wa masumbwi amestaafu, Pacquiao ni mkongwe na ana miaka 40 sasa anatakiwa kustaafu au nitamstaafisha,” aliongeza.

Maneno hayo yalionekana kumvuruga Pacquiao ambaye alijibu kwa kumueleza kuwa huwa anawazima kwa ngumi watu wanaomsema vibaya na kumtishia kwa mdomo. Alisema maneno hayo ni upuuzi na dharau.

“Siku zote mimi huwa siongei sana au kutoa maneno machafu (trash talk). Wengi huwa wanaongea sana, wanaahidi kuwa watanipiga vibaya, lakini tukishapanda ulingoni huwa inakuwa tofauti,” alisema.

Bondia huyo Mfilipino na Seneta wa jimbo la Sarangani alimuahidi bondia huyo mwenye umri wa miaka 30 kuwa watakapokuwa ulingoni atamuonesha kwa vitendo na atamtesa.

Pambano hili linavuta usikivu wa wapenzi wengi wa ndondi ulimwenguni kutokana na jinsi ambavyo Pacquiao ameamua kumchagua bondia kijana na machachari, Keith Thurman bila kujali tofauti ya umri.

Lugola awatumbua askari sakata la mahabusu kutoroka
Waziri Mkuu wa Uingereza atangaza kujiuzulu

Comments

comments