Jeshi la polisi nchini Kenya limemkamata mume wa mwanariadha maarufu na Bingwa wa Dunia mara mbili kwenye Olympics, Agnes Tirop, aliyekutwa amefariki dunia nyumbani kwake mjini Iten.

Mwanariadha huyo aliyekuwa na umri wa miaka 25 alikutwa akiwa amefariki dunia Jumatano wiki hii na mwili wake ulikua na majeraha ya kuchomwa kisu shingoni.

Katika ripoti yake, Tom Makori ambaye ni Kamanda wa Polisi wa Keiyo North alieleza jinsi walivyoukuta mwili wa mwanariadha huyo nyumbani kwake.

“Tulipoingia ndani ya nyumba, tulimkuta Tirop akiwa kitandani na kulikuwa damu nyingi iliyomwagika sakafuni. Tuliona alikuwa amechomwa na na kitu chenye ncha kali shingoni, ambacho tunaamini ni kisu,” alisema Makori.

Hata hivyo, hawakumkuta mumewe aitwaye Ibrahim Rotich na hakuwa anapatikana kwenye simu. Mazingira hayo yalisababisha kumfikiria kuwa ndiye mtuhumiwa wa tukio hilo.

Kifo cha mwanariadha huyo kimewaumiza wadau wengi na kuvuta usikivu wa dunia. RaiS wa Chama Cha Dunia cha Riadha, Sebastian Coe alituma salamu za rambirambi akieleza, “tasnia ya michezo imepoteza moja kati ya nyota bora katika mazingira ya kusikitisha sana.”

Mume wa Tirop alikamatwa jijini Mombasa, saa chache baada ya polisi kumtaka ajisalimishe.

“Mtuhumiwa amekamatwa leo jioni na yuko katika kituo cha polisi cha Changamwe katika Mkoa wa Pwani,” alisema Kamanda Makori.

Wakati huo, familia ya Tirop imeitaka Serikali kuhakikisha mali zote za ndugu yao zinarejeshwa mikononi mwao, kwani kila mali imeandikwa jina lake na la mumewe.

Sterling atishia kuondoka Mchester City
Serikali ya aahidi kutatua migogoro ya ardhi