Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati ametishia kuwatimua maajenti wa urais kutoka kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura cha Bomas of Kenya, hii leo majira ya alasiri, kwa kuchelewesha mchakato wa uhakiki.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), pia ilitangaza kuwa ili kuharakisha mchakato huo, maafisa wanaosimamia uchaguzi kuanzia sasa watachukua dakika 15 pekee katika ujazaji wa jedwali lolote la uthibitishaji.

Akisoma Sheria ya Kutuliza Ghasia kwa mawakala hao hii leo Agosti 12, 2022, Chebukati amewaonya maajenti hao kukoma kuwaingilia maafisa wake kupitia fomu zinazoletwa na wasimamizi wa uchaguzi.

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati akiongea wakati wa mkutano wake na Wanahabari Agosti 10, 2022. (Picha na Sila Kiplagat I Nation Media Group)

Aidha, amewataka mawakala hao kutowageuka wakaguzi wa kitaalamu, bali waangalie utaratibu na kuandika dosari ambazo watashirikiana kwa pamoja na si kuanzisha malumbano yanayosababisha ucheleweshwaji wa matokeo.

Amesema, “Zingatieni mchakato na hati lakini usifanye ukaguzi wa kisayansi wakati wa mchakato. Rekodi makosa yoyote na uripoti sawa. Iwapo nyinyi (maajenti) mna matatizo yoyote basi zungumza nami.”

Bosi huyo wa IEBC, pia amefafanua kuwa ili kuendelea mbele, mawakala wataangalia nakala za fomu na kuthibitisha kuwa ni sawa na zile zinazotolewa katika vituo vya kupigia kura.

Dkt. Mpango: Ajira za watoto Migodini zikomeshwe
Kenya: Mwingine akamatwa kwa upotevu wa masanduku ya kura