Polisi wa eneo la Loitoktok nchini Kenya, imesema mwili wa Afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Embakasi Mashariki, Daniel Mbolu Musyoka (53), aliyetoweka siku ya Jumatano Agosti 10, 2022, umepatikana ukiwa umetupwa pembeni ya bonde la mto wa kiangazi la Kajiado.

Mkuu wa kituo cha Polisi cha Loitoktok kaunti ndogo ya Kajiado Kusini, Kipruto Ruto amesema waliarifiwa kuhusu kuwepo kwa mwili wa mwanamume wa makamo uliokuwa katika eneo moja la msituni na baadaye ulitambuliwa na dada wa marehemu Mary Mwikali na Ann Mboya katika chumba cha kuhifadhi maiti cha kaunti hiyo.

“Dada zake wawili walitambua mwili huo ukiwa umehifadhiwa katika hospitali ndogo ya Loitoktok jana usiku (Agosti 14, 2022) na tunasubiri mawasiliano kutoka Makao Makuu ya Polisi ili kusafirisha mwili huo hadi katika eneo la kuhifadhi ya maiti la jiji au kama utasalia hapa,” amefafanua Ruto.

Marehemu Musyoka, alikuwa akihudumu kama msimamizi katika kituo cha kupigia kura cha Embakasi Mashariki katika kaunti ya Nairobi, na baada ya kutoweka mwili wake uligunduliwa na wafugaji hapo jana Jumatatu Agosti 15, 2022 katika msitu wa Kilombero, pembeni ya Mlima Kilimanjaro kwenye bonde la mto wa kiangazi.

Eneo la bonde la mto wa kiangazi, ulipopatikana mwili huo linatajwa kuwa maarufu kwa waathiriwa wa mauaji ambapo miili yao hupatikana ikiwa imetupwa, Mkuu huyo wa Polisi akisema mwili huo ulikutwa ukiwa mtupu na nguo zake (track suit na shuka la kimasai) vikipatikana kwenye ukingo wa bonde ukiwa na majeraha.

“Ni dhahiri kuwa marehemu aliuawa kwingine na mwili kutupwa hapo bondeni na tumeukuta mwili huo una makovu yanayoashiria kuteswa kabla ya kifo na uchunguzi wa awali unaonesha huenda alikufa kifo cha maumivu,” ameongeza Ruto.

Mwili huo ulihamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Loitokitok ukisubiri kutambuliwa baada ya maafisa wa Polisi kuchukua alama za vidole.

Marekani yamtaka Mteule Ruto kufanya kazi na washindani wake
Ahmed Ally: Wanaomlaumu Matoka hawajui Soka