Baadhi ya wafuasi wa ngome ya Raila Odinga iliyopo mjini Kisumu, wamesema wanatarajia kumuapisha Odinga kuwa Rais wa nchi hiyo ili Kenya iwe na Marais wawili na kwamba endapo watu hawataikubali hali hiyo wataomba Kenya igawanyike.

Mbali na kauli hiyo, pia wafuasi hao wamesema wanaikubali hukumu ya Mahakama ya Juu ya Kenya ya kutupilia mbali ombi la Odinga la kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti, uliomtaja mpinzani wake, William Ruto kuwa mshindi.

“Tutaapa ili Raila Amollo Odinga ndiye awe rais mteule ili tuwe na marais wawili na iwapo lolote litatokea tutaitisha kujitenga ili Kenya igawanywe.”

Wakihojiwa na vyombo mbalimbali vya Habari, Wafuasi hao wamesema wameikubali hukumu hiyo kwa kuwa ni wakongwe katika maisha ya nchi hiyo kwa kusema tatizo lililopo ni pesa ambayo inaipoteza nchi.

“Nitaikubali hukumu hiyo kwa moyo mkunjufu kwa sababu tumeishi Kenya hii na tumeona mengi, kuna tatizo moja tu la Kenya nalo ni pesa (akimaanisha rushwa) pesa inaipotezea nchi hii,” aliongea mmoja wa wafuasi hao.

Amesema, “Mahakama kuu imetoa uamuzi wake lakini nitasubiri jenerali wangu ambaye ni Raila Amollo Odinga atoe maelekezo ya wapi tunapita ikiwa hili litakuwa jaribio lake la mwisho, basi pia nitasema kuwa hii ni mara yangu ya mwisho kwenda kupiga kura.”

Raila Odinga. Picha na Leo leo Media.

Odinga, amekuwa akifurahia uungwaji mkono wa hali ya juu, hasa kutoka maeneo ya magharibi mwa Kenya na ameshindana zaidi ya mara tano katika chaguzi za Urais tangu 1997 na kila mara amekuwa akidai kuhujumiwa.

Kuchaguliwa kwa Ruto kuwa rais wa tano wa jamhuri ya Kenya kumezua ukosoaji toka kwa wafuasi wa Odinga, ambao wanasema “hatutamwita Ruto rais, tutamwita Raila Amollo rais, kama tulifanya 2017 hii ni sawa na tutafanya.”

Kenya, ndiyo nchi yenye uchumi unaoendelea zaidi Afrika Mashariki, lakini Taifa hilo limelaumiwa kwa kuwatesa raia wake, kutokana na bei za bidhaa za msingi kuwa juu na ukosefu wa ajira ukiwa ni tatizo umeota mizizi miongoni mwa vijana.

Kiongozi TFF aingilia sakata la Tuisila Kisinda
Denis Lavagne kocha mpya Azam FC