Wakati Wakenya wakisubiri kuandika historia ya kumshuhudia Rais wa 5, jamii ya Shona waliowasili Kenya mwanzoni mwa miaka ya 1960 wakitokea Zimbabwe wao wanafurahia kupiga kura kwa mara ya kwanza tangu Kenya ilipopata uhuru wake mwaka 1963.

Watu hao walikuwa wakiishi nchini humo bila utaifa hadi mwaka jana 2021 serikali ya Kenya ilipowapatia uraia kwa kuzingatia kampeni ya hivi karibuni ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR ya kutokomeza tatizo la ukosefu wa utaifa ifikapo mwaka 2024.

Miaka mitatu iliyopita, Serikali ya Kenya kwa kushirikiana na UNHCR na wadau wengine, iliwapatia vyeti vya kuzaliwa zaidi ya watoto 600 wa asili ya jamii ya Shona, na kuwa raia wa Kenya huku wazazi wao ambao wakisalia bila utaifa hadi mwaka 2021.

Mshona, Branjimeni Mshawa Ndooro aliyefanikiwa kupiga kura kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa Kenya baada ya kupatiwa uraia wa Taifa hilo mwaka 2021. Picha na Abdikarim Haji / UNIC Nairobi

Wanasema, “tumezaliwa hapa na sisi tumezaa watoto ndipo ikahitajika shuleni wajiandikishe wapate vyeti vya kuzaliwa na hapo ndipo tulipoanza kukutana na shida lakini wenzetu walitusaidia na Serikali, Umoja wa Mataifa na Kamisheni ya haki za binadamu wakaingilia kati.”

“Tunamshukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa huruma zake, Mungu alimgusa roho hii shughuli ikafanikishwa ili na sisi tujisikie kama wanadamu, kama wananchi wale wengine na sasa. tumeonja utamu wa kuwa raia,” wamesema baadhi ya washona nchini Kenya.

Washona walifika Kenya mwaka wa 1960 na kuishi kama watu wasio na utaifa kwa karibu miongo sita hadi Julai 28, 2021, walipotambuliwa kama kabila la 45 la Kenya wakiwa na stakabadhi zote zinazohitajika na walijiandikisha kupiga kura, na Jumanne, Agosti 9, 2022 wakashiriki zoezi la kura kwa mara ya kwanza kama raia wa Kenya.

Kenya: IEBC yapunguza kura elfu 10 za Ruto
Lori laziba barabara Morogoro