Kiongozi wa waangalizi wa Uchaguzi Mkuu wa Kenya kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka wagombea ambao hawatakubaliana na matokeo waende Mahakamani badala ya kutumia njia nyingine isiyo sahihi.

Kikwete, ametoa kauli hiyo hii leo Agosti 11, 2022 wakati akitoa ripoti ya awali juu ya mchakato wa uchaguzi ulivyokuwa hadi sasa, ambapo matokeo ya maeneo mbalimbali yamekuwa yakitolewa.

“Tunawasihi muendeleze amani na utulivu baada ya matokeo kutangazwa, kama mtu atakuwa na pingamizi kuna mwanya wa kisheria hivyo wachukue mkondo huo,” amesema Kikwete.

Amesema, uchaguzi umefanyika kwa amani, utulivu na uwazi zaidi kutokana na maandalizi yaliyofanywa na Taifa hilo, pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Uchaguzi wa mwaka 2017, Mahakama ya Juu nchini Kenya iliyafuta matokeo ya kura ya urais ya uchaguzi huo baada ya kukubaliana na hoja za mgombea urais, Raila Odinga za uwepo wa kasoro kwenye ukusanyaji na usafirishaji wa matokeo hayo. 

Makamu wa Rais ahimiza kilimo cha Biashara
Balozi Sokoine aongoza ujumbe wa Tanzania maandalizi mkutano wa SADC