Ni sawa na kusema nchi za Afrika sasa zimeshituka kutumia pesa nyingi kuwapatia wazungu wanaofundisha timu za taifa bila ya mrejesho mzuri wa mapesa hayo na sasa zimeanza kutumia makocha wazalendo kujaribu kupata mafanikio.

Kama ilivyo nchini Tanzania ambapo mzalendo Charles Bonface Mkwasa ‘Master’ ameaminiwa na watanzania kuifundisha timu ya taifa ya soka taifa stars, nchini Kenya Shirikisho la soka nchini humo limemtangaza Stanley Okumbi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa Harambee Stars.

Okumbi ambaye ni hivi karibuni tu aliachana na kazi ya kuifundisha Mathare United kabla ya kumalizika msimu wa 2015 anachukua nafasi ya Bobby Williamson raia wa Scotland ambaye alikuwa akiifundisha Harambee Stars kwa muda mwaka mmoja na nusu.

Kocha huyo wa zamani wa vilabu vya Mathare na Kariobangi Sharks ana wasifu wa kuwa na leseni ya ukocha ya shirikisho la soka barani Afrika CAF.

Atakuwa akisaidiana na nahodha wa zamani wa timu ya Harambee Stars Musa Otieno na Frank Ouna ambaye pia ni kocha msaidizi wa Gor Mahia.

Akiongea wakati wa utambulisho wake Jumamosi jijini Nairobi, Okumbi mwenye umri wa miaka 35, alimshukuru Rais mpya wa FKF Nick Mwendwa kwa kumuamini katika kazi hiyo na kuahidi kuitendea haki nafasi hiyo kwa kuibadilisha timu ya taifa ambayo kila mkenya atajivunia.

Mtihani wa kwanza wa Okumbi utakuwa katika mchezo dhidi ya Guinea Bissau mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika ugenini huko Bissau mwezi machi. Ameahidi timu ya taifa kucheza aina mpya ya uchezaji wake.

Harambee Stars inatarajiwa kuanza mazoezi ya maandalizi ya kampeni hiyo wiki ijayo.

 

Malinzi: Mwenye Ushahidi Aupeleke TAKUKURU
Twiga Stars Waendelea Kuwavutia Kasi Zimbabwe