Serikali ya Kenya imetangaza kufuta masharti ya watalii na wageni wengine kuwekwa karantini waingiapo nchini humo, isipokuwa kwa wale ambao wataonesha dalili za kuwa na virusi vipya vya corona (covid-19).

Akizungumza wiki hii jijini Nairobi, Waziri wa Usafiri wa Kenya, James Macharia amesema kuwa hatua hiyo imelenga katika kuhamasisha kurejesha ukuaji wa sekta ya utalii ambao uliathirika kwa kiasi kikubwa tangu covid-19 ilipotangazwa rasmi nchini humo Machi, 2020.

Amesema kuwa abiria watakaowekwa karantini ni wale tu ambao watakuwa wameonesha dalili kama kuwa na jotoridi zaidi ya 37.5, kikohozi kisichokoma, matatizo ya upumuaji na dalili nyingine za mafua.

Macharia ameongeza kuwa endapo itabainika kuwa kulikuwa na wagonjwa wa corona kwenye chombo cha usafiri kutoka nje, wafanyakazi wa chombo hicho watawekwa ‘karantini’ nyumbani na abiria wengine wenye dalili watafanyiwa vipimo zaidi.

“Pale ambapo kutakuwa na mtu anayedhaniwa kuwa na covid-19 kwenye ndege, wafanyakazi watawekwa ‘karantini’ nyumbani. Na itakapokuwa lazima, wafanyakazi hawataruhusiwa kutoka kwenye vyumba vyao hotelini isipokuwa wakati wa dharura,” amesema Waziri Macharia.

“Abiria wote hawatakuwa na ulazima wa kukaa karantini wafikapo nchini Kenya isipokuwa tu wale ambao jotoridi lao la mwili ni zaidi ya 37.5, na wenye matatizo ya kupumua au wenye dalili za mafua ya aina fulani ifananayo na corona. Hii ni muhimu kwa sababu hatutarajii mtalii anapokuja kutoka sehemu yoyote awekwe karantini kwa siku 14,” ameongeza.

Akitangaza maelekezo ya Rais Uhuru Kenyatta kuwa usafiri wa anga utarejea rasmi kuanzia Julai 15, 2020, amesema kuwa ndege tano pekee zimeshathibitisha kuwa zitaanza safari zake nchini humo.

Uamuzi wa Kenya unafuata nyayo za uamuzi uliofanywa na Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, alioutoa Mei, 2020. Rais Magufuli alisema ndege zote za watalii ruksa kutua nchini na kuelekea kwenye hifadhi za taifa kwa ajili ya kushuhudia uzuri wa Tanzania bila kuwa na sharti la kuwekwa karantini.

Rais Magufuli alisema kuwa baada ya kupimwa jotoridi la mwili, wageni hao wapewe taarifa kuwa mbali na kutalii wanaweza kupata huduma ya ‘kujifukiza’ maarufu kama ‘kupiga nyungu’, ambayo ni sehemu ya njia za kupambana na athari za covid-19.

JPM ateua Mkuu wa wilaya Nzega
Paul Pogba kusaini mkataba mpya Man Utd?